Kocha Mrundi agundua jambo Azam

Muktasari:

Bahati  kwa sasa anakaimu nafasi ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Aristica Cioba ambaye yupo nchini kwao Romania ambako kuna katazo 'Lockdown' la wananchi kuzurula nje bila sababu kutokana na uwepo wa janga la corona

KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Mrundi Bahati Vivier, ameona utofauti wa utimamu wa miili ya  wachezaji wake katika mazoezi yao ya kwanza ambayo wamefanya leo jioni kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini.

Bahati anakaimu kwa muda uongozi wa benchi la ufundi la Azam kutokana na kocha mkuu Aristica Cioaba kukwama Romania kwa sababu ya sheria ya kutotoka nje na kufungwa mipaka ambayo imewekwa ili kukabiliana na virusi vya Corona.

Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ambayo yalifanyika kwa saa moja, Vivier alisema anahitaji muda wa wiki mbili ili kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa katika kiwango sawa cha utimamu wa mwili.

"Unajua kila mmoja alikuwa akifanya mazoezi binafsi hivyo nilitarajia kuona utofauti. Kuna  wachezaji ambao wapo juu lakini wengine wapo chini hivyo ni jukumu langu kama kocha kulirekebisha ingawa wote kuwa sawa, inahitaji muda.

"Leo tumefanya mazoezi ya kawaida huku wakipeana nafasi wachezaji, program zitakuwa zikibadilika kwa muongozo wa kocha mkuu ambaye yupo Romania," alisema Vivier.

Kikosi cha Azam FC, kimeanza mazoezi rasmi leo ikiwa ni siku chache baada ya kuruhusiwa kuendelea kwa shughuli mbalimbali za kimichezo nchini ili kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara, inayotarajiwa kuendelea mwezi ujao, Juni, 2020.

Katika mazoezi hayo, wachezaji wa Azam walionekana kupeana nafasi ikiwa ni sehemu ya tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona licha ya kuwa hadi sasa hakuna Lisa chochote kwa wachezaji wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Upande wake Ofisa habari wa timu hiyo, Zakaria Thabiti 'Zaka za Kazi', alisema wakati ambao wachezaji walipokuwa wakiripoti kila mmoja alikuwa akipimwa joto lake la mwili.

"Bado hatujawapima corona lakini tumepima kila mmoja joto lake la mwili, wapo sawa kila mmoja na hakuna ambaye tulimtilia shaka," alisema Zakaria