Kocha Klopp: Nyie mnataka tusajili ili iweje?

Muktasari:

Msimu huu sasa mabosi wa Liverpool wamekausha tu, wanaziangalia tu klabu nyingine zinavyoshindana sokoni.

LIVERPOOL, ENGLAND.BAADA ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita huku wakiangusha vigogo kibao, Liverpool sasa wanajiamini ile mbaya.

Kocha wao, Jurgen Klopp ametamba hawana haja ya kumwaga pesa kusajili katika dirisha hili la uhamisho, maana wao hawamwagimwagi pesa ovyo kila mwaka kama Manchester City na PSG.

Liverpool ilishatumia mkwanja mrefu wa kuzinasa saini za wachezaji wa maana kama Alisson, Virgil van Dijk na Fabinho ambao mchango wao umeonekana katika kuleta taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuwabana koo City hadi siku ya mwisho katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England ambako ilimalimaliza katika nafasi ya pili.

Msimu huu sasa mabosi wa Liverpool wamekausha tu, wanaziangalia tu klabu nyingine zinavyoshindana sokoni.

Kufikia sasa imemsajili kinda Sepp Van den Berg mwenye umri wa miaka 16 kutoka Zwolle ya Uholanzi, huku pia kinda mwingine kutoka Fulham, Harvey Elliott akitarajiwa kutua hivi karibuni.

Kocha Klopp ana furaha kuingia katika msimu mpya wa 2019-20 na kikosi kilekile na akamwaga tambo kwamba hahitaji kumwaga pesa kila msimu.

“Hatuna presha katika hilo,” alisema Klopp. “Hatutafanya makubwa katika dirisha hili la uhamisho, tumeshatumia pesa nyingi kununua wachezaji katika misimu miwili iliyopita. Hatuwezi kuendelea kumwaga pesa kila msimu kama Barcelona, Real Madrid, Man City na PSG.

“Sisi tuko poa. Nina furaha na kikosi nilichonacho.”