Kocha Ihefu atimuliwa

Muktasari:

Mwalwisi aliipandisha timu hiyo Ligi Kuu kupitia hatua ya mtoano (Play Off) kwa kuitoa Mbao FC , na   ameiongoza katika  mechi tano za Ligi Kuu Bara na kuambulia pointi tatu 

Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Makka Mwalwisi amekuwa kocha wa kwanza msimu huu kuonyeshwa mlango wa kutokea baada ya  leo Jumanne kusitishiwa mkataba na mabosi wake kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Kocha huyo ambaye ameiongoza timu hiyo katika  mechi tano na kuambulia pointi tatu tu, amesema leo Jumatatu Oktoba 5, amepokea barua ya kusitishwa mkataba wake.

 Mwalwisi ambaye ameipandisha timu hiyo msimu huu, ameongeza kuwa kwa sasa anaenda kupumzika huku akisubiri ofa yoyote itakayokuja mezani kwake.

“Ni kweli leo nimepokea barua ya kusitishwa kwa mkataba wangu na kubwa zaidi ni matokeo.Mabosi wameangalia mwenendo wa timu na  hawajaridhika hivyo tumeachana salama” amesema Mwalwisi. Amefafanua kuwa kazi yake ni kufundisha mpira, hivyo hawezi kubagua wapi afanye kazi ispokuwa kama kuna timu yoyote  wataelewana yeye atapiga kazi na kuwatakia kila la kheri Ihefu.

Ihefu iko nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza michezo mitano , imeshinda mmoja na kupoteza minne.