Kocha: Yajayo Yanga yanafurahisha

Muktasari:

Kocha wa sasa wa AS Vita, Florent Ibenge amewaambia Yanga kwamba, jamaa ni kifaa na wakimpata watafurahia shoo yake.

YANGA wanakuna vichwa wakijiuliza wamchukulie uamuzi gani winga wao Bernard Morrison, ambaye bado ameikacha timu yao lakini wanapiga hesabu za kumchukua Emmannuel Ngudikama, ambaye ni staa wa zamani wa AS Vita aliyewahi kuwaumiza Simba katika kipigo cha mabao 5-0.

Kocha wa sasa wa AS Vita, Florent Ibenge amewaambia Yanga kwamba, jamaa ni kifaa na wakimpata watafurahia shoo yake.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu jana moja kwa moja kutoka jijini Kinshasa, DR Congo Ibenge ambaye pia anatajwa kusakwa kuja kukiwasha kwenye Ligi Kuu Bara, alisema; “Anajua kuchezesha timu kule mbele na anafunga pia. Hatulii ni mtu anayehangaika kutafuta ushindi wa timu. Nimefanya naye kazi kwa misimu mitano kabla ya kwenda Angola.”

Ibenge mwenye sifa ya upole, amewaambia Yanga kama wanamtaka Ngudikama basi wajipange kwani mshambuliaji huyo anapigiwa hesabu pia na DC Motema Pembe, AS Vita na Maniema Union ambao watashiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao.

“Emmanuel (Ngudikama) hataki kurudi tena Angola na kama Yanga wanamtaka basi wapambane na timu tatu za hapa Congo ambazo zinataka huduma yake.

Lakini, Ngudikama mwenyewe ameliambia Mwanaspoti kuwa anafahamu Yanga wanamtaka na anashawishika kukubali ofa ya timu hiyo baada ya kuzungumza na staa mwingine mpya ambaye Yanga atakayesaini muda wowote, Tuisila Kisinda.

“Kisinda ni rafiki yangu kila wiki lazima nionane naye, ameniambia Yanga watamsajili. Ukweli ni mchezaji mzuri sana ngoja tusubiri kuona kama mabosi wa Yanga watasema lolote.”