Koba Kimanga aeleza alivyotupa taulo pambano lake na Michael

Muktasari:

Koba anasema tukio hilo lilitokea mwaka 1985 katika michuano ya Klabu Bingwa Taifa iliyofanyika mkoani Mbeya na alitaja kuwa ni tukio ambalo hatasahau katika maisha yake ya ngumi.

Dar es Salaam Koba Kimanga ni miongoni mwa mabondia wachache wa uzito wa juu ‘heavy weight’ waliowahi kutokea nchini ambaye alitumia kipaji chake cha ngumi kuitangaza Tanzania.

Bondia mwingine wa uzito wa juu aliyewahi kuwika katika michuano mbalimbali ni Timothy Kingu ambaye kama Koba, alikuwa hodari wa kurusha makonde ulingoni.

Koba na Kingu wanaingia katika orodha ya mabondia waliowahi kutamba katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yaliyopata chati katika miaka ya 1980.

Unapozungumzia ubora wa Koba, huwezi kumuweka kando aliyekuwa bondia na kocha wa timu ya Taifa ya ngumi Nassor Michael.

Koba na Michael ambao kwasasa wamestaafu ngumi baada ya kuitumikia nchi kwa mafanikio, wana historia ya pekee katika mchezo huo.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, Koba anasimulia mkasa wa kusisimua kuhusu pambano lake na Michael mwaka 1985.

Katika ngumi miongoni mwa matokeo yanayotambulika ni yale ya kurushiwa taulo na msaidizi wako (second) aliyeko nje ya ulingo.

Msaidizi wako anaruhusiwa kufanya hivyo kwa lengo la kukunusuru na kipigo pale anapoona umezidiwa na makonde ya mpinzani wako.

Lakini kwa Koba hali imekuwa tofauti, yeye aligomea uamuzi wa msaidizi wake katika pambano lake na Michael.

“Niliporushiwa taulo na msaidizi wangu nililiokota na kulitupa nje nikamwambia mwamuzi naendelea na pambano,” anasimulia Koba.

Koba anasema tukio hilo lilitokea mwaka 1985 katika michuano ya Klabu Bingwa Taifa iliyofanyika mkoani Mbeya na alitaja kuwa ni tukio ambalo hatasahau katika maisha yake ya ngumi.

“Nilikuwa nacheza na Nassor Michael ngumi za ridhaa.Nassor alikuwa akijiandaa na mashindano ya jeshi, alikuja kwenye klabu yetu ya Simba Boxing kuomba ‘sparing’ na mimi, alinipiga lakini nilimsumbua na kabla ya kuondoka akamwambia kocha wangu huyu mtoto atakuwa mkali,” anasimulia Koba.

Anasema kocha wake Habibu Kinyogoli alimwambia asimuogope Michael ambaye alikuwa staa wakati ule hata ikitokea amepangiwa kucheza naye.

“Kwenye mashindano ya klabu bingwa kweli nikapangwa kucheza naye lilikuwa pambano la gumzo, Nassor alikuwa maarufu. Kila mtu alikuwa akinishangaa Willy Isangula (bondia wa zamani) aliniambia Koba jiandae kupigwa.

“Siku ya pambano naingia tu ukumbini mashabiki wakaanza kunishangilia, lakini si kwa ushindi waliona nimepatikana. Ilinibidi nikajifiche kwanza baada ya muda MC akatangaza pambano linalofuata ni Nassor na Koba wajiandae,” anakumbuka Koba.” anasema Koba.

Nini kilitokea baada ya mwamuzi kuashiria kuanza pambano hilo, fuatilia toleo lijalo.