Klopp amtetea beki wa Chelsea

London, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameshikwa na hasira baada ya baadhi ya wachezaji na mmoja wa benchi lake la ufundi kushangilia tukio la beki wa Chelsea, Andreas Christensen kuonyeshwa kadi nyekundu.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu England uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Stamford Bridge uliingia dosari dakika moja kabla ya mapumziko baada ya beki huyo wa kimataifa wa Denmark kutolewa uwanjani kwa kumvuta Sadio Mane.

Christensen alianza kuonyeshwa kadi ya njano kabla ya mwamuzi, Paul Tierney, kuuangalia tena marudio ya picha za video kwenye runinga iliyowekwa uwanjani na kubadilisha uamuzi wake.

Licha ya kuwa Liverpool ilitawala katika kipindi cha kwanza, kikosi cha kocha Frank Lampard kilikuwa bado mchezoni na kwenda mapumziko na matokeo ya 0-0.

Mane aliingia vizuri akitafuta nafasi ya kufunga bao la kuongoza kwa pasi

ya Jordan Henderson, kabla ya Christensen kumwangusha akiwa anaelekea kufunga.

Mwandishi wa soka wa Ufaransa, Julien Laurens aliripoti kuwa wakati Christensen akionyeshwa kadi nyekundu, wachezaji waliokuwa benchi wa Liverpool walikuwa wakipiga makofi kushangilia tukio hilo.

Tukio hilo lilimfanya kocha Klopp kuamka kwa hasira na kuwafokea wachezaji na kiongozi mmoja wa benchi la ufundi akisema: “Nyinyi ni vichaa? Kamwe hatufanyagi hivyo, sawa.”

Lakini baadaye, kocha huyo raia wa Ujerumani alifafanua: “hakuwa mmoja wa wachezaji wangu wa akiba, ni mmoja wa benchi la ufundi, na nilimwambia cha kufanya na si kushangilia. Si kitu ninachotaka kukiona.”