Klabu za Ligi Kuu zajazwa

Dar es Salaam. Benki ya KCB imeendelea kuwa mmoja wa wadhamini wa Ligi Kuu Bara baada ya kuongea mkataba wa mwaka mmoja utakaoifanya kila klabu kuambulia zaidi ya Sh16 milioni.

Mkataba huo umesainiwa jana Dar es Salaam na unaifanya KBC kuwa na msimu wa nne wa kudhamini Ligi Kuu Bara.

Udhamini huo utaigharimu benki hiyo Sh500 milioni kabla ya kukatwa kodi, mkataba ambao umekosa ongezeko kubwa na ule wa msimu uliopita sababu ikitajwa kuwa ni mdororo wa uchumi uliosababishwa na Covid 19.

Katika mchanganuo wa udhamini huo baada ya makato ya kodi, Sh425 kitabakia na kufanya kiasi cha Sh300 kwenda kwa mgao wa klabu 18.

Sh125 kitabaki katika gharama za utawala na uendeshaji huku mgao halisi utaifanya kila klabu kuambulia zaidi ya Sh16 milioni kwa mwaka huo.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa KCB, Barry Chale, ambaye alimuwakilisha mkurugenzi mkuu wa benki hiyo, alisema ushirikiano walioupata kutoka kwa TFF ndiyo matunda ya wao kuamua kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo hususan Ligi Kuu Tanzania Bara.

Chale alisema benki yao inaona mafanikio ya mpira wa miguu kwa ushindani unaoonekana na kwamba hatua yao hiyo inalenga kuunga mkono ajira kwa wachezaji na wafanyakazi wengine.

“Tanzania sasa kuna wachezaji wanacheza Ulaya, kwahiyo hii ni hatua kubwa na sisi KCB tunaona kwa muamko nasi tuungane na TFF katika kuhakikisha mpira unapiga hatua zaidi,” alisema Chale.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ya Tanzania (TPLB), Steven Mnguto, ambaye alimwakilisha Rais wa TFF, Wallece Karia, alisema kiasi kikubwa cha fedha hizo za udhamini zitakwenda moja kwa moja kwa klabu shiriki za Ligi Kuu Tanzania Bara.