Kitambi anafanya kisichotakiwa kufanywa

Muktasari:

Katika timu zinazoendeshwa kisayansi na kisasa, kocha mkuu huwa na benchi lake la ufundi. Akifukuzwa kazi, huondoka na wenzake wote aliokuwa nao. Hii ni kwa sababu, kama kikosi kina shida au kina mafanikio ni kwa sababu ya benchi nzima na si mtu mmoja mmoja.

WIKI hii nimekuwa nikisoma magazeti mbalimbali ya Tanzania na mitandao kuhusu maelezo yanayotolewa na Kocha Msaidizi wa Simba, Denis Kitambi, kuhusu mwenendo wa timu yake katika siku za karibuni.

Nakubali kwamba simfahamu Kitambi kiundani Zaidi ya kupewa maelezo ya hapa na pale kutoka kwa watu wanaofahamu au waliowahi kufanya naye kazi. Mmoja wa waandishi wa habari vijana aliwahi kunieleza kwamba Kitambi ni mmoja wa walimu wachache wazalendo wanaojua kuhusu misingi na miiko ya kazi hapa nchini. Mwandishi huyo alikwenda mbali na kuniambia kwamba tabia zake hizo ndizo zimekuwa mojawapo ya sababu zinazomfanya ashindwe kufanya kazi na timu za Tanzania ambazo bado zina ‘Uswahili’ mwingi.

Nikiri kwamba ninachokisoma magazetini na mitandaoni kinanipa maswali mengi kuhusu maelezo niliyopewa na mwandishi huyu kumhusu Kitambi. Kwa mtazamo wangu, anachokifanya Kitambi ni kitu kilicho kinyume kabisa na maelezo niliyopewa.

Ninafahamu kwamba Patrick Aussems hakumleta Kitambi awe msaidizi wake. Sidhani kama alikuwa anajua chochote kumhusu kabla hajaanza kazi Tanzania. Hata hivyo, katika kazi hizi, watu hufanya kazi kama timu moja.Ndiyo maana nilishangazwa sana niliposikia Kitambi akihojiwa na kuzungumzia kuhusu wachezaji wa Simba kukata pumzi kipindi cha pili na pia kwamba wachezaji wamepoteza morali. Haya si mambo ambayo Kocha Msaidizi anayazungumza wakati bosi wake akiwa kikaangoni. Ni aina nyingine ya usaliti.

Katika timu zinazoendeshwa kisayansi na kisasa, kocha mkuu huwa na benchi lake la ufundi. Akifukuzwa kazi, huondoka na wenzake wote aliokuwa nao. Hii ni kwa sababu, kama kikosi kina shida au kina mafanikio ni kwa sababu ya benchi nzima na si mtu mmoja mmoja.

Kama timu ilikuwa inakata pumzi kipindi cha pili, hili si ni suala la mwalimu msaidizi kubuni namna ya kufanyisha mazoezi ambayo yataongeza tija? Kama wachezaji hawana morali, si ni jukumu la wasaidizi wa kocha mkuu kuzungumza na wachezaji mmoja mmoja kujua nini ni kiini cha tatizo husika?

Nimefanya kazi kwenye magazeti kwa Zaidi ya miaka 15 na mara nyingi gazeti kuwa baya si tatizo la Mhariri Mkuu peke yake ingawa yeye anabeba lawama. Kuna sababu za ndani na nje ambazo husababisha gazeti kuvutia au kutovutia. Na mzigo wa lawama haupaswi kuangukia mezani kwa mtu mmoja.

Nafahamu kwamba Denis ana matamanio yake ya kitaalamu kwenye ukocha lakini naamini anaweza kuyapata pasipo kuonekana kama msaliti mbele ya Aussems.

Mimi nimefanya kazi na walimu wa kigeni wakati nikiwa kiongozi wa Simba na ninafahamu kwamba huwa wanawasiliana na kupeana siri mbili tatu. Jambo moja ambalo huwa hawasamehi ni usaliti au kugeukwa na wasaidizi wao.

Nakumbuka sana tukio moja la namna hii. Simba ilitoka kufukuza kazi kocha mmoja wa kigeni na akaja mwingine. Huyo alipokuja, hakuwa na masharti sana lakini wiki mbili baadaye, akaja kutaka aliyekuwa msaidizi wake ambaye alimkuta aondolewe. Nikaja kuambiwa alitonywa na mtangulizi wake.

Kama Aussems atakuwa anaambiwa nini kinachozungumzwa na msaidizi wake huyo kwenye mahojiano rasmi na vyombo vya habari, atakuwa ni mtu mwenye hasira sana.

Haya ni mambo ambayo huko walikotoka hayapo.

Jurgen Klopp aligombana na rafiki yake na msaidizi wake wa zaidi ya miaka 20, Zeljko Buvac, kwa sababu alifanya mazungumzo ya kujiunga na klabu nyingine na Klopp akajua pasipo kuambiwa na rafikiye huyo. Akaamua kumuondoa kwenye benchi lake la ufundi.

Mauricio Pochetino amefukuzwa na Spurs na timu ilikuwa inaonekana ina matatizo lakini umesikia nini kutoka kwa wasaidizi wake? Uliwahi kusikia chochote kutoka kwa wasaidizi wa Arsene Wenger alipoondoka zake Arsenal au wasaidizi wa Jose Mourinho wakati anafukuzwa Manchester United? Ni kimya tu.

Na ukimya huu unasaidia kwa sababu kama Aussems, kwa mfano tu, akiwa amempenda Kitambi, anaweza kuamua kwenda naye kwenye nchi nyingine ya Afrika endapo atapata fursa ya kufundisha. Ipo stori kumhusu Sir Alex Ferguson namna alivyojuana na Mreno, Carlos Quieroz, katika siku zake za mwisho za ukocha na kutamani wangefahamiana mapema.

Tanzania kama nchi ina namna mbili za kutoa makocha wenye kufundisha nje ya mipaka yetu. Njia ya kwanza ni kama ile ya Dennis Kitambi alipokwenda Kenya kufundisha na njia ya pili ni kupitia mteremko wa kuwa wasaidizi wa makocha wenye kujulikana na kupewa kazi nje ya nchi.

Lakini, njia hii ya pili itafanya kazi endapo makocha wetu watajitahidi kuwa weledi na kufanya mambo yatakayowafanya wageni hawa kuwaona wanafaa kuwa wasaidizi wao katika majukumu mengine makubwa. Njia hii anayopita Dennis Kitambi kwa Aussems si njia sahihi. A

ussems anaweza kuwa na makosa ya kusababisha kufukuzwa kazi lakini kanuni za kazini zinatufundisha jambo moja kuhusu uhusiano baina ya mtu na bosi wake.

Kanuni yenyewe inasema, “A boss is always right.”