Kisa lafudhi Ronaldo ageuka kituko darasani

Tuesday December 3 2019

Kisa -lafudhi -Ronaldo- ageuka- kituko- darasani-mwandishi- Luca- Caioli -Messi -mahakamani-mchezaji-baba-mwanasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

KATIKA toleo lililopita, mwandishi, Luca Caioli aliichambua kashfa ya Messi kukwepa kodi hadi kufikishwa mahakamani na namna jambo hilo lilivyomweka katika wakati mgumu mchezaji huyo pamoja na baba yake. Sasa endelea…

Baada ya hapo kilichofuata ni kwa mamlaka za usimamizi wa fedha Hispania kuanza uchunguzi wa tuhuma zilizowekwa wazi na Panama Papers, ukweli kuhusu hilo haukuweza kuthibitishwa.

Yote kwa yote sifa na hadhi ya Messi ikawa kama imetingishwa kwa mara nyingine kuhusu utata huo wa mambo ya fedha ukihusisha ukwepaji wa kodi.

Kama ilivyo kwa Messi, Ronaldo naye alipitia wakati mgumu katika maisha yake ya soka hasa miaka michache ya mwanzo, Ronaldo alikumbana na changamoto kama za Messi.

Mreno huyu aliondoka Madeira na kuachana na familia yake akiwa ndio kwanza ana miaka 12 ili kuifukuzia ndoto yake ya soko katika Jiji la Lisbon kwenye klabu ya Sporting Lisbon.

“Lilikuwa jambo gumu kweli, ni kipindi kigumu zaidi katika maisha yangu kwenye soka,” anakumbukwa Ronaldo kuwahi kusema baadaye.

Advertisement

“Mama yangu na dada zangu walikuwa wakilia, nami nilikuwa nikilia, nililia hata wakati nikiwa kwenye ndege na ndio kwanza ndege ilikuwa imeanza kuondoka, nilianza kuifikiria familia yangu ilivyokuwa ikinililia, name nikaanza kulia tena.”

Siku ya kwanza akiwa shule ilikuwa mbaya na ya ovyo. Ronaldo alichelewa kuingia darasani na mwalimu tayari alikuwa ameshachukua majina ya wanafunzi wote, wakati akisimama na kuanza kutaja jina lake alisikia baadhi ya wanafunzi waliokaa nyuma wakimcheka kutokana na lafudhi yake ya Madeira.

Lafudhi hiyo ilikuwa tofauti na ile iliyozoeleka kwa Wareno wengi wa Jiji la Lisbon makao makuu ya nchi, ni kama vile alikuwa akizungumza kwa lafudhi tofauti na iliyozoeleka, alionekana kama mtu kutoka kisiwa cha mbali na hakuna ambaye alimwelewa.

Alikasirika na kutishia kumpiga mwalimu wake kwa kiti, akawa mfano wa kituko darasani, na akajiona wa hovyo wakati huo huo kumbukumbu za nyumbani zikaanza kumjia, akaanza kupakumbuka Madeira, akawakumbuka marafiki zake.

Alikuwa akipiga simu nyumbani mara mbili au tatu kwa wiki, alisikitika mno kusikia sauti ya mama yake, hali hiyo ilimfanya aanze kulia na kumkumbuka zaidi.

Dolores (mama yake Ronaldo) alikuwa akijaribu kumbembeleza akimtaka awapuuze wanaomtania na kumdharau shuleni, kuna wakati alikuwa akimshawish na kumuaminisha kwamba maisha yake na mambo yake yote ya baadaye yako Lisbon katika shule ya soka la klabu ya Sporting Lisbon.

Mwisho wa yote mama huyo alilazimika kwenda Lisbon kwa sababu mtoto wake alimwambia kwamba ameshindwa kuvumilia, anataka kuondoka kuachana na ndoto zake za soka na kurudi nyumbani ili tu awe karibu na familia yake.

Ulikuwa mwaka wa kwanza mgumu lakini hatimaye alizowea maisha na sasa anakiri kwamba amefanya jambo kubwa na kupata uzoefu.

“Katika kipindi kigumu unajifunza mengi kuhusu wewe mwenyewe,’’ alisema Ronaldo. “Unatakiwa kuendelea kuwa imara na kuweka mkazo katika kile unachokitaka.”

Alihitaji uimara huo katika miaka mingine mingi iliyofuata ili kumsaidia kuendana na kipindi cha huzuni katika maisha yake.

Itaendelea Jumamosi ijayo…

Advertisement