Kisa Simba, ratiba Yanga yabadilika

Muktasari:

Yanga na Kagera Sugar zimekutana mara mbili msimu huu ambapo kila moja imeibuka na ushindi dhidi ya nyingine

Homa ya mechi ya mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, imepelekea kubadilishwa kwa ratiba ya mechi ya Ligi Kuu baina ya Kagera Sugar na Yanga.

Mchezo huo wa Kagera Sugar na Yanga uliokuwa uchezwe kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, Julai 9, umerudishwa nyuma na sas utachezwa Jumatano, Julai 8.

Taarifa za kubadilishwa kwa ratiba ya mechi hiyo zimenaswa kupitia barua ambayo Bodi ya Ligi Kuu imeiandika kwenda Kagera Sugar kuwataarifu juu ya mabadiliko hayo.

"Bodi ya Ligi inapenda kukutaarifu kuwa mchezo tajwa hapo utachezwa tarehe 08.07.2020 saa tisa (9) mchana katika uwanja wa Kagera Sugar FC mkoani Kagera badala ya tarehe 09.07.2020 kama ilivyokuwa hapo awali.

Sababu ya mabadiliko haya ni kuipa timu ya Young Africans SC muda wa kujiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho (FA)," ilifafanua barua hiyo.

Mchezo huo ni wa tatu kwa Yanga na Kagera Sugar kukutana msimu huu ambapo mara ya kwanza ziliumana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu lakini pia zikakutana kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Jumanne, wiki iliyopita.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu zilipocheza kwenye Uwanja wa Uhuru, Januari 15, Yanga ilichapwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Yusufu Mhilu, Ally Ramadhan na Peter Mwalyanzi.

Kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Juni 30, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, yaliyofungwa na David Molinga pamoja na Deus Kaseke huku lile la Kagera likifungwa na Awesu Awesu.