Kisa Corona! Messi kukatwa mshahara

Muktasari:

Kutokana na agizo la kusitisha La Liga, mapato ya Barcelona yameyumba huku ikikosa mapato ya vifaa vya michezo na viingilio.

BARCELONA, HISPANIA . KATIKA kuunga mkono vita dhidi ya virusi vya Corona, wachezaji wa Barcelona akiwemo Lionel Messi, wako tayari kupokea nusu mshahara kama watatakiwa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa AS, baada ya viongozi wa wachezaji kufanya kikao na Rais Josep Maria Bartomeu, walisema hawatakuwa na pingamizi kama hilo litatokea.

Septemba mwaka jana, Wakurugenzi wa Barcelona walitangaza kuwa itakuwa klabu ya kwanza kuvuka kikwazo cha kiuchumi, lakini hiyo itazingatia kama wataingiza fedha za kutosha.

Kutokana na agizo la kusitisha La Liga, mapato ya Barcelona yameyumba huku ikikosa mapato ya vifaa vya michezo na viingilio.

Lakini kutokana na tatizo la Corona, mechi hazipo na hivyo mapato yamesimama na hilo limeanza kuwatia hofu ya kuyumba kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni, kuahirishwa kwa mechi ya Ligi ya mabingwa dhidi ya Napoli, kuliigharimu klabu hiyo zaidi ya Pauni 5.5 milioni.

Msimu uliopita nyumba ya maonyesho iliingiza Pauni 55 milioni huku duka la kuuuza jezi, ikiingiza Pauni 79 milioni.

Sheria za soka nchini Hispania, zinaruhusu klabu kukata mshahara wa wachezaji, mpaka pale tatizo lililosababisha maamuzi hayo kuisha.