Kipigo cha Shakhtar, Zizou ajibebesha lawama

Thursday October 22 2020
zizou pic

MADRID, HISPANIA. KOCHA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amejibebesha lawama ya kipogo cha ambacho kikosi chake wamekumbana nacho kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetsk huku akisema ulikuwa mchezo mbovu na usiku mbaya kwao kuelekea El  Clasico, Jumamosi.

Real Madrid ilijikuta ikiwa nyuma kwa mabao 3-0 kwenye uwanja wa Alfredo di Stefano baada ya kufanya makosa mengi kwenye safu yao ya ulinzi ambayo ilimkosa nahodha wao, Sergio Ramos kabla ya kuzinduka kipindi cha pili.

Vijana hao wa Zizou, walipambana kipindi cha pili na kupata mabao mawili kupitia kwa

  Luka Modric na  Vinicius Junior  lakini mabao hayo, hayakutosha kuwafanya wasikumbane na kipigo kwenye mchezo huo.

Matokeo hayo, yanatajwa kuingeza presha kwa Real Madrid kuelekea kwenye mchezo wa watani wa jadi Hispania 'El Clasico' ambao unatarajiwa kuchezwa wikiendi ijayo huko Camp Nou huku Barcelona wakiwa wenyeji.

"Tulifanya kosa kwenye bao la kwanza na baada ya hapo tukapoteza uwezo wetu wa kujiamini. Lakini wachezaji wangu walizinduka kipindi cha pili," amesema kocha huyo raia wa Ufaransa mara baada ya mchezo huo kumalizika.

Advertisement

Hakuishia hapo, ameongeza kuwa," Ulikuwa mchezo mbovu na usiku mbaya kwetu.Mimi ni kocha natakiwa kutafuta utatuzi ambao kwenye huu mchezo sikuupata."

"Hatukucheza inavyotakiwa lakini pamoja na hilo kikubwa kilikuwa ni kupoteza uwezo wa kujiamini kwa wachezaji wangu. Ni siku nyingine mbaya kwetu, kwa sasa tunapaswa kujiandaa na mchezo ujao," amesema.

Real Madrid wameuanza msimu wa 2020-21 kwa sare na ushindi kwenye mchezo mitatu mfululizo kabla ya kukiona cha mtema kuni wikiendi iliyopita na sasa wapo mbele ya pointi tatu dhidi ya wapinzani wao kwenye La Liga ambao wapo mchezo mmoja nyuma.

"Matokeo ya namna hii yanafanya wachezaji wasiwe na furaha ambao walinifanya kushinda kila kitu, hawastahili hiki lakini ndio maisha ya mpira yalivyo huu ni kama usiku kwetu lakini kesho jua litachomoza tena," amesema.

Ramos ambaye alikosekana kwenye mchezo huo kutokana na majeraha, anatarajiwa kurejea kwenye mchezo ujao dhidi ya Barca.

 

 

MATOKEO MENGINE

Ajax 0-1 Liverpool

Bayern 4-0 Atletico Madrid

Inter Milan 2-2 B. Monchengladbach

Man City 3-1 Porto

Midtjylland 0-4 Atalanta

Olympiacos 1-0 Marseille

Advertisement