Kipese: Ushindi Taifa Stars upo kwa Yondani, Farid

Muktasari:

Tanzania inashika nafasi ya mwisho katika Kundi C lenye timu za Algeria, Senegal na Kenya

Dar es Salaam.Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' itacheza mchezo wa pili katika Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), Kundi 'C' dhidi ya Kenya mshindi katika mchezo huo atajiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa 16 bora Afrika.

Akizungumzia mechi hiyo mchezaji wa zamani wa Yanga na Simba, Thomas Kipese alisema ushindi wa Taifa Stars leo upo eneo la kiungo na eneo la ulinzi.

Katika eneo la kiungo Taifa Stars mechi iliyopita alicheza Mudathir Yahaya, Feisal Salum aliyetolewa na kuingia Farid Mussa pamoja na Himid Mao na katika eneo la ulinzi wa mabeki wa kati alianza Kelvin Yondan na David Mwantika.

Kipese alisema kama viungo watafanya kazi yao vizuri ya kukaba na kuanzisha mashambulizi kwa maana ya kutengeneza nafasi za kufunga tutapata mabao, lakini katika eneo la ulinzi wanatakiwa kupunguza makosa ambayo walifanya kwenye mchezo uliopita na Senegal.

"Niliwaona Kenya kwenye mechi yao ya kwanza na Algeria walicheza vizuri kulikoa Taifa Stars walivyocheza na Senegal kwa maana hiyo tunakwenda kukutana na timu ambayo ni nzuri na kama tutashindwa kubadilika kwa kufanya makosa yale yale ya mchezo uliopita tutafungwa tena," alisema Kipese.

"Wachezaji pamoja na benchi la ufundi wanatakiwa wanakwenda kukutana na timu yenye wachezaji imara ambao si wa kuwafanyia mzaha wala makosa ya mara kwa mara ambayo watatumia kutuadhibu, lakini nafasi ambazo zitapatikana za kufunga katika mchezo wa leo tunatakiwa kuzitimia vizuri," alisema Kipese.