Kipa Sofapaka atuzwa mchezaji bora

Muktasari:

  • Ndikumana alimpiku Bethuel Warambo wa KCB, Enosh Ochieng wa Ulinzi Stars na Eric Kapaito wa Kariobangi Sharks kwenye orodha ya wachezaji waliowasilishwa mwezi huo.

MLINDAMLANGO wa Sofapaka Justin Ndikumana ametajwa mchezaji bora wa mwezi Machi na chama cha waandishi wa habari za spoti nchini.

Ndikumana, raia wa Burundi anakuwa golikipa wa pili kuwahi kushinda tuzo hiyo baada ya Gabriel Andika aliyetuzwa siku zake Western Stima mwaka 2015.

Ndikumana alimpiku Bethuel Warambo wa KCB, Enosh Ochieng wa Ulinzi Stars na Eric Kapaito wa Kariobangi Sharks kwenye orodha ya wachezaji waliowasilishwa mwezi huo.

Ili kuwahi tuzo hilo, alizuia kutofungwa mara tatu kwenye mechi nne za mwezi Machi.

“Nilikuwa naomba sana nituzwe maana nilicheza vizuri sana mwezi huo yaani kila mtu alikuwa akinipongeza hivyo nawashukuru kamati ya wanahabari kwa zawadi hii itakayonituma nitie bidii Zaidi,” alisema.

Anajiunga na kocha wake John Baraza aliyetuzwa kocha bora wa mwezi jana Batoto ba Mungu wakilenga ubingwa wa msimu huu.

“Najihisi naweza kumenyana na mpinzani yeyote sasa hivi na nitazidi kusaidia timu yangu kutimiza malengo yake msimu huu ya kuwahi ubingwa,” aliongeza.

Ndikumana ni mmoja wa nyota wa timu ya taifa ya Burundi itakayoelekea katika fainali za mataifa bora barani (AFCON) kule Misri timu yake ikiwa imepangwa kundi B pamoja na Nigeria, Madagascar na Guinea.

“Mwanzo tunajivunia kuandikisha historia kufuzu mashindano haya sasa hatuendi kushiriki tu bali kushindana na matumaini ya kuandikisha historia nyingine ya kusonga raundi ya pili,” alimalizia Ndikumana aliyejiunga na Sofapaka msimu huu kutoka St Eloi Lupopo ya Kongo.