Kipa Cameroon agoma kustaafu
Muktasari:
Kameni alikuwa sehemu ya kikosi cha Cameroon kilichotwaa Ubingwa wa AFCON mwaka 2002, baada ya hapo aliliongoza taifa lake kushika nafasi ya pili katika Kombe la Mabara.
KIPA wa Timu ya Taifa ya Cameroon, Carlos Iddris Kameni amesema, pamoja na kuvuliwa ubingwa wa fainali za mataifa ya Afrika hana mpango wa kustaafu soka kwa sasa.
Kipa huyo mwenye miaka 35, amekuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Cameroon katika awamu sita tofauti za fainali za AFCON, ikiwemo hii inayoendelea kutimua vumbi nchini Misri.
“Sifikirii kustaafu soka kwa sasa. Najiona mwenye nguvu za kuendelea kucheza, pia taifa langu bado linanihitaji, nipo tayari kupigania namba pamoja na vijana wanaochipukia,” alisema Kameni .
Kameni, ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa kwenye klabu za Espanyol na Malaga, kabla ya kwenda Uturuki kuichezea Fernabache alisema, wamepata somo kufuatia kushindwa kwao kutetea ubingwa wa AFCON.
“Tulienda Misri kutetea ubingwa wetu, tulikuwa na imani kubwa ya kufanya hivyo, kilichotokea hatukukitegemea na tumekipokea kama somo ambalo litatusaidia mbeleni,” alisema kipa huyo.
Wakati huo huo, kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Misri, Hassan Shehata ameelekeza lawama zake kwa Mapharao na shirikisho la soka nchini humo (EFA) kwa kuondolewa kwa timu hiyo ya taifa katika fainali za mataifa ya Afrika.
Shehata ambaye ndiye aliyeinoa timu hiyo ya taifa, iliyolibakisha kombe hilo kwenye ardhi yao ya nyumbani mwaka 2006, alisema alitarajia kufanya vibaya kwa timu hiyo.
“Nilibashiri tangu walipocheza mchezo wa kwanza kwamba hawawezi kufika popote. Kama ningekuwa kocha kwenye kundi la wachezaji walioitwa basi ningechukua watano tu, achana na (Mohamed) Salah na (Mahmoud Hassan) Trezeguet hao si tatizo vipi kuhusu wachezaji wengine,” alisema Shehata.