Kindoki asema ushirikina ulitaka kumng’oa Yanga

Muktasari:

  • Wachezaji wenzake walikuwa wakihoji kuhusu ubora wa kiwango chake baada ya kuporomoka ghafla licha ya kuanza vyema.

Dar es Salaam. Nyota aliyebadili upepo katika kikosi cha Yanga na kuonekana bora ni kipa Klause Kindoki raia wa DR Congo.

Kindoki wakati anajiunga na Yanga alionekana anakuja kuwa kipa namba moja, lakini ghafla upepo ulibadilika na kuonekana si mali.

Kipa huyo hakukubalika baada ya kiwango chake kuporomoka na kuonekana mzigo kwa Yanga.

Mashabiki wa Yanga walimzonga Kindoki na kumuona hana maana baada ya kufungwa mabao mepesi.

Ghafla kiwango chake katika mechi mbili ikiwemo ya Kombe la FA dhidi ya Namungo Yanga iliyoshinda bao 1-0 kabla ya kusimama imara walipoifunga Alliance mabao 2-1.

Kindoki anasema alianza kuhisi mabadiliko ya kiafya na kupoteza uimara wa kusimama langoni.

“Nilikuwa najishangaa kutokana na hali ile, unajua mimi najijua ubora wangu lakini kila kitu nilichokuwa nafanya nilikuwa kama naanza upya,”anasema Kindoki.

Anasema wachezaji wenzake walikuwa wakimfuata na kumpa imani asiwe na presha na walimtaka kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii.

Kindoki anasema wachezaji wenzake walikuwa wakihoji kuhusu ubora wa kiwango chake baada ya kuporomoka ghafla licha ya kuanza vyema.

Ushirikina

Anasema kutofanya vyema katika mechi za Yanga kuliwaibua baadhi ya wadau wa klabu hiyo ambao walimtaka kwenda ‘upande wa pili’.

Kipa huyo anasema baadhi yao waliamini kufanya vibaya huenda kuna mkono wa mtu katika imani za kishirikina.

“Sikuwa naamini kama hilo lipo ingawa kila nilipokutana na watu, mashabiki na baadhi ya wachezaji walikuwa wananiambia kuna ushirikina nimefanyiwa.

“Kuna mambo ambayo siwezi kuongea kwa vyombo vya habari kuwa walikuwa wanamtaja mtu aliyenifanyia.

“Hilo liliniumiza nikakosa furaha na kazi yangu tatizo nililibaini hapa Tanzania wachezaji wengi ni wazuri lakini wanapenda sana kuendekeza imani za kishirikina,” anasema Kindoki.

Mchezaji huyo anasema baadhi ya wachezaji wenzake walikuwa wakimwambia kuhusu masuala ya ushirikina alipokuwa katika kipindi kigumu.

Hata hivyo, pamoja na mazungumzo hayo, Kindoki aligoma kuweka wazi kama alikwenda kufanyiwa dawa au vinginevyo ili kurejesha kiwango chake.

Kindoki anasema ana amini kiwango chake kimerejea baada ya kumuomba Mungu na kuongeza bidii katika mazoezi.

Lugha

“Kingine kilichokuwa kinanisumbua awali ni kutojua vyema lugha ya kuwasiliana na wenzangu, hapa wanatumia sana kiswahili sikuwa najua kuzungumza lugha hii lakini baada ya kuchukua hatua ya kujifundisha nikaweza kuongea na wenzangu hasa mabeki,” alisema Kindoki.

Mashabiki

“Wakati ambao nilikuwa sifanyi vizuri kitu kilichokuwa kikiniumiza zaidi ni pale mashabiki walipokuwa wananishamb ulia kwa maneno makali hasa kwa timu yangu, lakini hata baadhi ya viongozi nao nikashangaa wakisema mimi ni kipa mbovu niondolewe.

“Nashangaa sasa mashabiki hao wamebadilika wanaona nafanya vizuri kila nikipita wanasema nadaka kama nyani wengine wanasema Kindoki anadaka kama De Gea nashangaa.

Kindoki anasema baada ya kufanyiwa vitimbi alikataa tamaa, lakini baada ya kumuomba Mungu na kurejesha kiwango chake, hana mpango wa kuondoka Yanga.

“Kwasasa naona kiwango changu kimebadilika naona anarudi Kindoki ninayemjua lakini bado sijafika pale ninapotaka muda unavyokwenda nitakuwa sawa” anasema Kindoki.

Ubingwa

Mchezaji huyo anasema Yanga ni timu bora licha ya kukumbwa na msukosuko, lakini ana matumaini itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Anasema anataka kutoa mchango wake Yanga kwa kucheza kwa umakini  katika lango lake kwa kuwa ana uwezo wa kudaka.

Yanga inaongoza kwa pointi 67 ikifuatiwa na Azam 59 na Simba 51 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tuna nafasi ya kufanya vizuri tutaendelea kuhakikisha kila mechi tunashinda lakini kuchukua makombe naona hili Kombe la FA ni lazima tutalichukua,

“Tumebakiza mechi tatu kuchukua taji hili tutapambana lipo ndani ya uwezo wetu,” anasema Kindoki.