Kimewaka VPL, mbona watalia wengi sana

LIGI Kuu Bara hadi sasa kila timu imecheza michezo mitano na umeshuhudiwa ushindani mkubwa ukitawala kwa timu kusaka alama tatu.

Wageni wameanza kwa kasi kucheka na nyavu tofauti na msimu uliopita wazawa walijitahidi kwenye eneo hilo. Mambo yamekuwa magumu pia kwa timu zilizopanda hazijaonyesha ushindani kama ilivyokuwa Polisi Tanzania na Namungo FC msimu uliopita. Mwanaspoti linakuletea mambo kadhaa ambayo hadi sasa yameonekana kwenye michezo iliyopigwa huku ukisubiri kuona mapambano yakiendelea wikiendi ya Novemba 7 wakati Yanga ikiikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkapa.

VITA YA MAKIPA

Hadi sasa kila timu imecheza michezo mitano, lakini imeshuhudiwa kipa wa Yanga, Metacha Mnata ndiye hajaruhusu bao langoni mwake baada ya kucheza michezo minne.

Yanga ilianza ligi kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkapa wakati langoni akiwapo Farouk Shikhalo na baada ya Mkenya huyo kuumia mazoezini, kocha akawa anamwanzisha Metacha ambaye hajaruhusu bao na kuifanya timu kuruhusu bao moja pekee.

Kagera Sugar wamemvurugia David Kissu kwenye mchezo wao pale Chamazi baada ya dakika 90 kumalizika kwa Azam kushinda 4-2. Kabla ya mchezo huo Kisu alikuwa hajaruhusu bao lolote.

Aishi Manula ameruhusu mabao mawili wakati Simba ikishinda 2-1 mbele ya Ihefu SC kisha sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar. Vita hiyo inachangiwa na wote kuitwa kwenye kikosi cha Stars na kuzidi kumpa ugumu kocha Etienne Ndayiragije ampange nani.

UFUNGAJI BORA

Kijana kutoka Zimbabwe, Prince Dube kaanza kwa kasi na kuwapoteza wale ambao walikuwa wamezoweleka kwenye ligi ya Bongo. Ni msimu wake wa kwanza lakini anafanya makubwa, ana kasi, analijua lango, anajua kupiga krosi, anapiga chenga na hadi sasa ndiye kinara wa mabao akiwa amefumania nyavu mara tano.

Meddie Kagere, mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa misimu miwili amerejea kwa kasi ile iliyozoweleka na mashabiki wa Simba na hadi sasa amefunga mabao manne.

Mshambuliaji mwingine wa kutazamwa msimu huu ni Chris Mugalu. Ukitaka jamaa asifunge basi mfunge kamba au asicheze kabisa, kwani tangu ametua Msimbazi michezo yote aliyocheza amefunga hata ile ya kirafiki. Hadi sasa ana mabao matatu.

Hao ndio washambuliaji watakaotazamwa zaidi msimu huu katika mchakamchaka wa kuwania ufungaji bora wa msimu huu na kumfanya Kagere kuzidisha kasi ya kutetea kiatu chake.

VICHAPO VIKALI

Hadi sasa timu iliyokula kichapo kikali ni 4-0. Septemba 7 - siku ya pili tu wakati ligi ikianza KMC iliichapa Mbeya City kwa mabao ya Emmanuel Mvuyekure, Hassan Kabunda, Abdul Hillary na Paul Peter.

Septemba 21, Simba nayo iliilaza 4-0 Biashara United kwa mabao ya Clatous Chama aliyefunga mawili, Kagere na Mugalu wakifunga bao mojamoja.

Oktoba 10, JKT Tanzania ikiwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ililala 4-0 mbele ya Simba kwa mabao ya Kagere aliyefunga mawili, Mugalu na Luis Miquissone wakifunga bao mojamoja.

Siku hiyo hiyo Azam iliichapa 4-2 Kagera Sugar kwa mabao ya Dube aliyefunga mawili, Obrey Chirwa na Richard Djodi bao mojamoja huku yale ya Kagera yakifungwa na David Luhende na Yusufu Mhilu.

MECHI BAO

Hadi sasa hakuna bao la penalti katika michezo yote iliyopigwa, lakini bao la kujifunga lipo moja lililoipa ushindi Coastal Union la Edson Katanga wa JKT Tanzania wakati timu yake ikifungwa bao 1-0 na Coastal Union.

Katika michezo ambayo imepigwa hadi sasa Dube ndiye mfungaji aliyetupia bao dakika za usiku wakati Azam ikiichapa 2-0 Coastal Union ambapo alifunga dakika ya 89, huku bao la mapema likiwa lile la Kagere katika dakika ya nne walipoichapa JKT Tanzania.

ZLATKO ATIA GUNDU

Aliyekuwa Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic alitua nchini Agosti 29 na kuanza kazi Agosti 30 akifanya kazi kwa siku 35 na Oktoba 3 alifungashiwa virago.

Zlatko amekuwa kocha wa kwanza msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara aliyedumu kwa muda mfupi, na msimu uliopita alikuwa Athuman Bilali ‘Billo’ aliyetimuliwa ikiwa siku ya kwanza tu alipoiongoza Alliance FC kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbao FC. Timu hizo zote zilishuka daraja.

Moja ya sababu zinazoelezwa kumtimua kocha huyo ni pamoja na mbinu na kugomea kikao na mabosi. Inaelezwa wakati Yanga ikimaliza mchezo wa ushindi wa pili kule Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar, Krmpotic alitaka kugomea kikao na viongozi wa klabu hiyo ambapo mabosi wanadaiwa kukitofasiri kuwa ni dharau.

Vilevile lugha isiyofaa kwa wachezaji wakati Yanga ikiwa Bukoba kucheza na Kagera Sugar inapoelezwa kuwa alimtolea maneno yasiyo na staha winga Farid Mussa hatua ambayo iliwakera wachezaji wenzake.

DUBE, MUGALU NOMA

Hawa jamaa noma sana! Ukitaka wasifunge basi usiwape nafasi ya kuingia uwanjani, kwani hata dakika mbili kwao watakuacha na maumivu makali.

Mugalu amecheza michezo mitatu ya ligi na tayari ametupia mabao matutu - akiwafunga JKT Tanzania, Gwambina na Biashara na amecheza michezo miwili akiwachapa Africans Lyon na Vital’ O

Dube naye aliwachapa bao mbili Coastal Union na Kagera na pia alitupia bao moja mbele ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

FUNGIA VIWANJA

Hadi sasa Bodi ya Ligi imevifungia viwanja vitano ikianza na Karume - Mara unaotumiwa na Biashara United kisha ukafuata ule wa Gwambina. Siku chache baadaye iliupiga pini Uwanja wa Mabatini unaotumiwa na Ruvu Shooting, kisha wa Ushirika unotumiwa na Polisi Tanzania na baadaye Jamhuri, Morogoro.

Sababu kubwa ya kufungiwa viwanja hivyo ni ubovu hasa eneo la kuchezea na vyumba vya kubadilishia nguo huku baadhi ya wadau wakionekana kuitupia lawama TFF kutokana na kitendo hicho.