Kilichowakumba Matola na Amri Said mbona utacheka!

Friday January 12 2018

 

By DORIS MALIYAGA

UKISIKIA sakata la makocha wa Lipuli wa Iringa,  Amri Said na Seleman Matola ambao ni marafiki wa kutupwa, mbona unaweza ukacheka mpaka.

Iko hivi, Amri anatambulika na TFF ndiye kocha mkuu kwa sababu ana leseni B na Matola mwenye leseni C  ni msaidizi wake, lakini kwenye timu, inadaiwa Matola ndiyo mkuu anayeandaa programu zote na Amri ni msaidizi tu.

Sasa bwana waliporudi kwenye timu kwa ajili ya maandalizi  ya mechi za ligi kuu wakitokea kwenye mapumziko kupisha kombe la Mapinduzi, Amri si akalianzisha bwana.

Inadaiwa wakati wako kwenye mazungumzo kuhusu maendeleo ya timu Amri ametoa kauli zinahusu program za timu kama yeye ndiyo bosi, jambo ambalo Matola hakufurahishwa nalo.

Unaambiwa Matola alikasirika na kuamua kufunga safari ya kurudi Dar es Salaam kuendelea na mipango yake mingine na kuiacha timu ikiendelea na maandalizi, lakini baada ya kumsihi na Amri kumweka sawa swahiba wake huyo, leo hii alianza safari ya kurudi Iringa.

"Kwa sasa kila kitu kinakwenda sawa, walikuwa wametofautiana kidogo Matola na Amri, unaweza kusema ni mambo ya kiuongozi tu lakini wale ni marafiki wameyamaliza,"anasema rafiki wa karibu wa makocha hao.

"Hili tukio inawezekana kabisa, kulikuwa na maneno ya chinichini ya kuwatofautisha lakini kwa sababu wanajuana vizuri, wameyazungumza na kuyamaliza, hivi tunavyoongea Matola yuko ndani ya basi anarudi Iringa kwa ajili ya kuendelea kuifundisha Lipuli na kesho mechi na Mtibwa atakuwa kwenye benchi."

Lipuli inacheza na Mtibwa Sugar kesho Jumamosi kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Samora.