Kilichomuondoa Aussems, kitawaondoa wengine Simba

Muktasari:

Katika kufuatilia kwa muda mrefu tangu kuibuka kwa uvumi wa kutaka kutimuliwa kwa Aussems ambaye msimu uliopita aliipeleka Simba hadi hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni mengi yamezungumzwa juu yake.

MBELGIJI Patrick Aussems ameondolewa kwenye ajira ya kuifundisha Simba kutokana na sababu mbalimbali zilizoelezwa na vigogo hao wa Ligi Kuu Bara. Kocha huyo tayari ameondoka nchini akiacha ujumbe wa kufikirisha kwenye akili zetu.

Aussems ametoa tuhuma nzito kuhusu Bodi ya Wakurugenzi wa Simba alipoandika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii kwamba katika “Bodi ya Klabu ya Simba kuna waongo na vilaza.”

Ni tuhuma nzito. Na kwa sababu amerusha jiwe gizani, mwenye kuelewa atakuwa ameelewa. Yaani hapa kila mmoja aelewe kivyake kulingana na uelewa wake.

Kwa sasa uongozi umeanza mchakato wa kumsaka kocha mpya akiwamo msaidizi wake Denis Kitambi ambaye pia inadaiwa kuwa ataondolewa na nafasi yake itachukuliwa na Seleman Matola.

Katika kufuatilia kwa muda mrefu tangu kuibuka kwa uvumi wa kutaka kutimuliwa kwa Aussems ambaye msimu uliopita aliipeleka Simba hadi hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni mengi yamezungumzwa juu yake.

Baadhi ya mambo yaliyozungumzwa ingawa mengi viongozi hawajayaweka wazi ni kocha huyo kutokuwa na ushirikiano mzuri na wenzake ikiwamo tuhuma za kudharau baadhi ya mambo aliyokuwa akielekezwa na mabosi wake.

Kushindwa kudhibiti suala la nidhamu kwa wachezaji ikidaiwa kwamba alikuwa anawatetea baadhi ya wachezaji wenye utovu wa nidhamu hivyo kuigawa timu.

Lililowekwa wazi zaidi ni kocha huyo kushindwa kufikia malengo ya klabu ikiwemo kuondoshwa mapema timu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali wakati lengo lao lilikuwa ni kufika makundi.

Aussems ameondolewa akiwa anaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara licha ya Simba kuwa na mechi tatu mkononi, wakiwa wamepoteza mechi moja na kutoka sare moja jambo ambalo kwenye ligi si baya sana kulingana na ushindani uliopo. Lakini hili haliwezi kuwa sababu ya msingi sana ya kuondolewa kwake labda kama kati ya zile sababu zinazodaiwa zilikuwa zimesababisha kufikia idadi.

Sababu hizo zinanifikirisha zaidi kwani ndani ya Simba makocha wengi wameondolewa kwa sababu zinazofanana hasa ikiwamo hiyo ya nidhamu mbovu, kugawa wachezaji na kuingiliwa kwenye majukumu yake ingawa kwa Aussems hili halijasikika kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Pengine lilikuwapo ila huenda alikuwa msiri nalo na alilivumilia kulinda kibarua chake ambacho hatimaye hata hivyo imeshindikana kukilinda.

Sawa. Simba watapata kocha mwingine atakayesaidiana na Selemani Matola, lakini je mfumo wao utakuwaje kuepusha suala la kugawa wachezaji, tatizo ambalo naliona linaanzia kwenye uongozi wenyewe? Je, suala la nidhamu kwa wachezaji wa Simba limeanza leo ama ni la siku zote? Kwenye hivi vitu viwili viongozi wanatakiwa kutafuta tiba halisi vinginevyo hata hawa wapya hawatadumu.

Na suala la nidhamu linasimamiwa na kocha au viongozi? Kama ni viongozi kwanini halijawahi kupatiwa ufumbuzi kwani ni la muda mrefu hata kabla ya Aussems kutua na kuondoka Simba?

Ni kweli pengine Aussems alikuwa na udhaifu ambao umewakera viongozi wake kama inavyodaiwa timu kushuka kiwango jambo ambalo pia linachangiwa na wachezaji wenyewe kwamba anapokuwa na nidhamu binafsi basi kila kitu kitakuwa sawa, lakini kama nidhamu yake ni ya kuongozwa na mtu basi kiwango ni lazima kishuke.

Nadhani kuna haja kwa mabosi wa Simba kuliangalia hili kwa undani zaidi ili wanakoelekea kwenye kupigania ubingwa ambao wanataka kuutetea wasije wakajivuruga na kuambulia patupu kutokana na mabadiliko hayo.

Kama kweli Denis Kitambi ataondoka ambaye alitolewa huko Kenya alikokuwa na ajira yake, basi Matola naye awe makini maana anaifahamu Simba vizuri tangu alipoichezea na kuifundisha kwa nyakati tofauti.

Matola ni kocha mzuri, lakini ndani ya Simba kama siku wakiamua kufanya jambo lao basi ubora wake hautaonekana kama ilivyo kwa makocha mbalimbali waliopita hapo ikiwemo hata yeye jinsi alivyoondoka wakati huo.

Ni wakati wake sasa Matola kuitumia nafasi hiyo vyema akiwa ndani ya Simba. Asikubali kuendelea kuwa kocha msaidizi bali ifikie hatua awe kocha mkuu kwa kwenda kujiendeleza kwenye kozi ambazo zitamuwezesha kupata leseni ya kusimama kama kocha mkuu.

Matola asikubali makocha wengine kupata mafanikio makubwa kupitia mgongo wake kutokana na kazi kubwa anayoifanya, maana siku Simba watakapoamua kufanya yao ni wazi hakutakuwepo na sifa zaidi ya kutuleza udhaifu mwingi wa kwanini wameachana naye.

Makocha wengi wanatajwa lakini mmoja tu ndo anahitajika ambaye atafanyiwa usaili kama ilivyokuwa kwa Aussems, atapita kwenye usajili lakini je yale yote yanayotakiwa ndani ya Simba atayaweza kuyatekeleza?

Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa amepewa kazi ya kusaka kocha huyo, lakini kwa muundo wa Simba inanipa shaka kwamba siku kocha huyo akifeli kwenye utendaji wake wa kazi basi hata yeye (Senzo) atakuwa amefeli na huenda wasione umuhimu wake pia kuendelea kuwemo kwenye nafasi hiyo. Hii ndio Simba buana.