Kila bao ni kicheko tu huko EPL

Muktasari:

Kwa rekodi za msimu uliopita, staa Gylfi Sigurdsson alifunga mabao 13, lakini mshahara wake wa mwaka huko Everton ni Pauni 5.2 milioni. Paul Pogba, naye alifunga mabao 13 kwenye ligi, huku mshahara wake ukiwa ni Pauni 15.08 kwa mwaka.

LONDON, ENGLAND. UNAAMBIWA hivi, mpira ni pesa. Soka zuri huleta pesa, lakini ni biashara yenye gharama kubwa pia.

Klabu za soka zimekuwa zikivunja benki kuonyesha kwamba wamepanga kunasa wachezaji wa thamani kubwa bila ya kuwa na uhakika kwamba kufanya hivyo kuwahakikishia mafanikio.

Kwa mfano, Manchester United imelipa Pauni 89 milioni kumrudisha kiungo Paul Pogba kwenye kikosi chao, lakini staa huyo wa Mfaransa hadi sasa bado anapambana kujitengenezea mashabiki, hajawakosha nyoyo bado.

Wanasoka bora wanalipwa mishahara mikubwa, lakini je inaendana na kile wanachokifanya ndani ya uwanja? Kwa mujibu wa takwimu za livefootballtickets.com hii ndio thamani ya pesa walizolipwa wachezaji kwa kulinganisha mabao waliyofunga kwa msimu uliopita kwenye Ligi Kuu England. Kwa kuchukua mastaa 15 waliokuwa vinara wa mabao msimu uliyopita, hii ndio gharama walizogharimu timu zao kwa kila bao kutokana na mishahara yao waliyolipwa kwa msimu wote.

Kwa rekodi za msimu uliopita, staa Gylfi Sigurdsson alifunga mabao 13, lakini mshahara wake wa mwaka huko Everton ni Pauni 5.2 milioni. Paul Pogba, naye alifunga mabao 13 kwenye ligi, huku mshahara wake ukiwa ni Pauni 15.08 kwa mwaka.

Straika Glenn Murray alifunga mabao 13 na mshahara wake ulikuwa Pauni 1.56 milioni kwa mwaka, wakati staa wa Arsenal, Alexandre Lacazette alifunga mabao 13 pia na mshahara wake wa mwaka ni Pauni 9.47 milioni.

Nyota wengine waliofunga mabao 13 ni Raul Jimenez wa Wolves na mshahara kwa msimu huo alilipwa Pauni 2.13 milioni, wakati Richarlison huko Everton alifunga mara 13 pia na mshahara wake kwa mwaka wote ulikuwa Pauni 4.68 milioni.

Callum Wilson alifunga mabao 14 na mshahara wake ni Pauni 2.08 milioni, wakati staa wa zamani wa Chelsea, Eden Hazard alifunga mabao 16 na mshahara wake kwa mwaka ulikuwa Pauni 11.7 milioni huko Stamford Bridge.

Fowadi wa Manchester City, Raheem Sterling alifunga mabao 17 na mshahara wake wa mwaka huko Etihad ulitajwa kuwa Pauni 9.36 milioni, huku mshambuliaji wa Tottenham Horspur, Harry Kane amefunga mabao 17 pia na mshahara wake wa mwaka ni Pauni 10.4 milioni.

Straika wa Leicester City, Jamie Vardy alifunga mabao 18 na mshahara wake wa mwaka ulikuwa Pauni 7.28 milioni, wakati fowadi wa Man City, Sergio Aguero alifunga mabao 21 na mshahara wake wa mwaka analipwa Pauni 13 milioni.

Supastaa wa Liverpool, aliyebeba Kiatu cha Dhahabu sambamba na wakali wengine wawili, Sadio Mane na Pierre-Emerick Aubameyang kutokana na kila mmoja kufunga mabao 22 kwenye Ligi Kuu England, lakini tofauti yao ilikuwa kwenye mishahara yao ya mwaka.

Mo Salah kwa mwaka huduma yake huko Etihad imewagharimu Pauni 10.4 milioni, sawa na ilivyowagharimu Arsenal kwenye kumlipa Aubameyang mshahara wake wa mwaka mzima, huku Mane amewagharimu Liverpool Pauni 5.2 milioni kwa mwaka.

Baada ya takwimu hizo, hapo sasa zinapatikana pesa halali ambazo klabu ililipa kwa kila bao walilofunga mastaa wake hao na hivyo kufanya kuwapo na wachezaji waliozigharimu mamilioni ya pesa kwa kulinganisha mishahara wanayolipwa na idadi ya mabao waliyofunga kuzipa ushindi timu zao.

Supastaa Pogba ndiye mchezaji ambaye aliigharimu timu yake pesa nyingi zaidi kwa kila bao alilofunga, kwamba Man United walinunua bao la staa huyo Pauni 1,160,000 kwa rekodi za kwenye Ligi Kuu England kwa msimu wote uliopita.

Hazard na mabao yake huko Chelsea, kila moja liliwagharimu The Blues Pauni 731,250 kwa kila bao alilofunga, wakati Lacazette bao lake moja liliwagharimu Arsenal Pauni 728,252, huku Aguero aliwachanja Man City Pauni 619,048 kwa kila bao na Kane wa Spurs, kila bao moja alilofunga kwenye Ligi Kuu England, liliigharimu timu yake Pauni 611,765 kutokana na mshahara wake aliolipwa kwa msimu wote wa 2018/19.

Sterling kila bao lake alilofunga liliigharimu Man City, Pauni 550,588, wakati staa wa kimataifa wa Gabon, Aubameyang huko Arsenal kila bao aliloweka kambani kwenye ligi, lililikuwa na gharama ya Pauni 472,727.

Mo Salah bao lake lilikuwa na thamani ya Pauni 472,727 huko Liverpool, wakati Vardy kila bao lake aliwachanja Leicester City, Pauni 404,444

na Sigurdsson aliwakamua Everton Pauni 400,000 kwa kila bao alilofunga, huku Richarlison pia aliwagharimu wababe hao wa Goodison Park Pauni 360,000 kila bao alilofunga.

Fowadi wa Liverpool, Sadio Mane kila bao alilofunga Ligi Kuu England lilikuwa na thamani ya Pauni 236,364 kutokana na mshahara wake wa mwaka mzima, wakati Raul Jimenez aliwagharimu Wolves Pauni 164,000 kwa kila bao, huku Callum Wilson aliigharimu Bournemouth Pauni 148,571 kwa kila bao alilofunga kwenye ligi na Glenn Murray aliichanja Burnley Pauni 120,000 kila bao alilofunga.

Straika veterani, Murray ndiye mchezaji ambaye bao lake lilikuwa na thamani ndogo kwa msimu uliopita ukilinganisha na wakali wengine 15 walioongoza kwa kufunga kwenye Ligi Kuu England.