VIDEO: Kikwete afichua kilichomkwamisha Manji Yanga

Muktasari:

  • Manji aliuzulu uenyekiti wa Yanga mnamo Machi 12, 2018 akidai kuwa anatoa nafasi kwa watu wengine kuiongoza.

Rais wa awamu ya nne ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete jana amefichua siri ya aliyewahu kuwa mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji kufeli mpango wake wa kuikodi klabu hiyo.


Akizungumza katika hafla ya utilianaji saini wa mkataba wa ushauri wa mfumo wa uendeshaji wa klabu baina ya Yanga na La Ligi jana jijini, Rais Kiwete alisema kuwa Manji alishindwa kutoa maelezo yanayoeleweka juu ya mpango wake.


Rais Kikwete alisema hilo halikumkwamisha Manji pekee bali hata katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, George Mpondela 'Castro' ambaye alikuwa wa kwanza kutoa wazo la kubadilisha mfumo wa uendeshaji.
"Matamanio ya mabadiliko katika Yanga katika mfumo wa uendeshaji ni yamuda mrefu sio ya leo. Mtakumbuka wakati wa katibu mkuu George Mpondela 'Castro'. Alikuja na Yanga Kampuni. Hilo jaribio kubwa la kufanya mabadiliko ya uendeshaji kwenye klabu.


La pili alipokuwa mwenyekiti Ndugu Yussuf Manji alipokuja na ile dhana ya kukodisha.Katika majaribio makubwa hili ni la tatu kwa kumbukumbu zangu, mengine yalikuwa ni mabadiliko ya katiba tu," alisema Rais Mstaafu Kikwete.


Rais Kikwete alisema kuwa Manji na Mpondela walikuwa na nafasi kubwa ya kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa Yanga lakini uwasilishaji wa mapendekezo yao haukuwa mzuri.
"Majaribio mawili ya kwanzahayakufanikiwa na yalileta mgawanyiko katika klabu. Lile la Castro lilikuwa na Yanga Kampuni na Yanga Asili. Na ilikuwa vurumai kwelikweli.


Castro alikuwa anakuja kwangu mara kwa mara nimkamuambia sikiliza mimi sina uongozi pale wewe kamalizane na viongozi wenzako na wanachama wenzako. Nia yake ilikuwa nzuri lakini lile jambo lenyewe halikueleweka.


Hata ndugu yetu Yussuf Manji alipokuja na wazo la kukodisha, nalo likaleta mgawanyiko mkubwa. Kuna waliokuwa wanakubali klabu akodishwe na kuna waliokuwa hawataki kabisa kusikia klabu kukodishwa," alisema Rais Kikwete.


Rais Kikwete alisema kuwa anaamini mabadiliko yanayotaka kufanywa sasa ndani ya Yanga yatafanyika kwa ufasaha.
"Naona safari hii tofauti, Tofauti ya kwanza, uongozi umewekeza katika matayarisho. Kwa maana ya kuwa na watu rasmi wanaofanya utafiti kwanza wa changamoto zinazoikabili klabu na haja ya kutafutia majawabu na watu wale wanasema kuwa katika kutafuta majawabu, jawabu linaweza kuwa ni hili.


Lakini la pili ambalo ninalona linafanyika vizuri ni kutafuta ushauri kwa watu wenye maarifa zaidi na uzoefu wa masuala ya uendeshaji wa klabu na masuala yanayohusu mpira wa miguu," alisema Rais Mstaafu Kikwete.