Kikosi cha ubingwa cha Leicester City kinavyosambaratika

Tuesday September 10 2019

 

LEICESTER,ENGLAND.LEICESTER City waliishtua dunia mwaka 2016 wakati walipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mbele ya vigogo.

Hata hivyo, kikosi cha wababe hao kilichotwaa ubingwa wa England kinaelekea kusambaratika kwa sasa.

Kasper Schmeichel (Bado yupo)

Akiwa amejiunga na Leicester City miaka mitano kabla ya ubingwa huo, Kasper alifuata nyayo za baba yake, Peter Schmeichel kwa kutwaa ubingwa huo msimu wa 2015/16 huku akiwa ameruhusu mabao 36 tu katika kampeni yote.

Kwa sasa katika umri wa miaka 32, Kasper ni miongoni mwa mastaa wachache waliotwaa ubingwa ambao bado wanaunguruma klabuni hapo. Ameichezea Leicester City zaidi ya mechi 332 sasa.

Danny Simpson (Ameondoka)

Advertisement

Kinda wa zamani wa Manchester United ambaye aliibuka kuwa mchezaji mkubwa Leicester City na kuwa mlinzi wa kudumu upande wa kulia wa mabingwa hao. Mkataba wake na Leicester City ulimalizika dirisha kubwa lililopita. Alipoteza nafasi yake kwa mlinzi wa kulia wa Kireno, Ricardo Pereira ambaye ameitendea haki nafasi hiyo. Kwa sasa Simpson anafanya mazoezi na kikosi cha West Brom kilichopo daraja la kwanza akiwa na matumaini ya kupewa mkataba.

Robert Huth (amestaafu)

Mlinzi wa kati wa Kijerumani ambaye kwa kiasi kikubwa aliwabadilisha Leicester City na kuwa mabingwa katika msimu wake wa kwanza kamili klabuni hapo baada ya awali kucheza kwa mkopo katika msimu wa pili wa 2014/15. Huth ambaye alikuwa akishirikiana na Wes Morgan katika safu ya ulinzi alimaliza mkataba wake katika dirisha kubwa la mwaka jana na kuamua kustaafu soka. Mjerumani huyu aliyeletwa katika Ligi Kuu ya England na Chelsea alicheza mechi 322 za Ligi Kuu ya England kwa jumla. Ametwaa ubingwa wa England mara tatu.

Wes Morgan (Yupo)

Mlinzi huyu wa kati aliyekuwa nahodha na kubeba kombe la kwanza la Ligi Kuu ya England mwaka huo alikuwa anajiandaa kuondoka Leicester City dirisha kubwa lililopita lakini akasaini mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuwasili kwa Kocha Brendan Rodgers aliyehitaji uzoefu wake. Morgan ameendelea kuwa mchezaji muhimu kikosini na msimu uliopita alicheza mechi 22 huku akifunga mabao katika mechi dhidi ya Burnley na Bournemouth.

Christian Fuchs (Yupo)

Mmoja kati ya wachezaji wanaopendwa na mashabiki. Staa huyu wa kimataifa wa Australia alikuwa mmoja kati ya wachezaji wa kudumu katika kikosi cha kwanza cha Kocha Claudio Ranieri akitamba katika ulinzi wa kushoto. Huo ulikuwa msimu wake wa kwanza klabuni. Hata hivyo, kwa sasa Fuchs amepoteza nafasi yake kwa mlinzi, Ben Chilwell ambaye amekuwa akitamba vilivyo klabuni hapo na hakuna shaka anastahili kucheza. Fuchs ataruhusiwa kuondoka bure mwishoni mwa msimu huu na inadaiwa anataka kujiunga na klabu moja ya Ligi Kuu ya Marekani.

Riyad Mahrez (ameondoka)

Alinunuliwa na Leicester City akitokea katika klabu ya Le Havre ya Ufaransa huku akiwa hana jina kubwa. Wakati huo Leicester City walikuwa wakicheza Ligi daraja la kwanza. Baadaye Mahrez aliibuka kuwa tishio na kuwa mmoja kati ya mastaa walioipa Leicester City ubingwa wa Ligi Kuu huku akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa England. staa huyu wa Algeria alibakia klabuni hapo kwa misimu miwili zaidi kabla ya kuishawishi Manchester City kuvunja rekodi yao ya uhamisho kwa kutoa Pauni 61 milioni dirisha kubwa la mwaka jana na kumng’oa Leicester. Alikichezea kikosi cha Kocha Pep Guardiola mechi 42 na kufunga mabao 11 huku akipika mengine 11 na kutwaa taji la England kwa mara nyingine akiwa na timu tofauti.

Danny Drinkwater (ameondoka)

Ungeweza kuwataja wachezaji watatu muhimu zaidi Leicester City iliyotwaa ubingwa na bado usingemtaja Danny Drinkwater. Hata hivyo alikuwa moyo katika safu ya kiungo ya kocha, Claudio Ranieri. Kinda huyu wa zamani wa Manchester United aliichezea Leicester City mechi 218 katika kipindi cha miaka mitano lakini mwaka 2017 akatua Chelsea. Hata hivyo mambo yamekwenda ovyo kwa Drinkwater na makocha wawili wa Chelsea, Maurizio Sarri na mrithi wake, Frank Lampard hawakumkubali kabisa kikosini hapo. Kwa sasa amekwenda Burnley kwa mkopo.

N’Golo Kanté (Ameondoka)

N’Golo Kanté aliichezea Leicester City msimu mmoja tu huo huo wa ubingwa akitokea Caen ya kwao Ufaransa mwaka 2015 kwa Pauni 8.1 milioni tu.

Hata hivyo, aliacha alama kubwa klabuni hapo baada ya kuisaidia Leicester kutwaa taji hilo. Mwishoni mwa msimu alihamia Chelsea kwa Pauni 36 milioni ambalo ni mara nne ya dau ambalo Leicester City walimnunua. Akaisaidia Chelsea pia kuchukua taji huku akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka England. Mwaka 2018 akaisaidia Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia 2018.

Marc Albrighton (Yupo)

Hakuwa mchezaji mwenye jina kubwa zaidi kuliko kina Mahrez lakini alikuwa mchezaji muhimu na hatari hasa kwa mipira ya adhabu. Aliongeza kitu tofauti katika safu ya ushambuliaji. Mpaka leo, staa huyu (29) ni mchezaji muhimu kikosini na amesaini mkataba mpya ambao utamweka klabuni hapo mpaka mwaka 2022.

Shinji Okazaki (Ameondoka)

Wakati akicheza Bundesliga katika klabu ya Mainz, Shinji Okazaki hakuwa hatari sana kwa ufungaji lakini ni jitihada zake akiwa hana mpira ndizo ambazo ziliishawishi Leicester City kumnunua kwa Pauni 10 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2010. Hata hivyo, Okazaki aligeuka kuwa tishio katika ufungaji na kusaidia kupika mabao wakati alipotua katika kikosi hicho akicheza sambamba na Jamie Vardy.

Aliondoka klabuni hapo dirisha kubwa lililopita la majira ya joto akitimkia katika klabu ya Malaga ya Hispania lakini klabu hiyo ikatangaza kushindwa kuendelea naye kutokana na ufinyu wa bajeti yao na ndani ya Mwezi tu Okazaki akatimka na kwenda katika klabu nyingine ya Huesca.

Jamie Vardy (Yupo)

Akitokea katika klabu ya mchangani ya Stocksbridge mpaka Leicester City, huku akipitia vipindi vya mkopo katika klabu za Halifax na Fleetwood, ndani ya miaka miwili tu, Vardy aligeuka kuwa mmoja kati ya washambuliaji tishio Ulaya.

Aliipandisha timu hiyo daraja huku akifunga mabao 16 pia akaipa ubingwa kwa mabao yake muhimu msimu huo akifunga mabao 24. Msimu uliopita alitakiwa na Arsenal lakini akaamua kubakia klabuni hapo. Mpaka sasa yupo katika timu akiongoza mstari wa mashambulizi klabuni hapo.

Leonardo Ulloa (Ameondoka)

Alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi huku akitokea xaidi katika benchi. Baada ya misimu mwili alikwenda kwa mkopo Brighton kisha akauzwa jumla kwenda Pachuca ya Mexico lakini sasa nyota huyu wa Kiargentina anakipiga katika klabu ya Rayo Vallecano.

Andy King (Ameondoka)

Kiungo huyu alikuwa jiwe muhimu akitokea zaidi katika benchi. Kuanzia pale, King amepelekwa kwa mkopo katika sehemu tatu. Alianzia Swansea, kisha Derby County na sasa yupo Rangers ya Uskochi.

Alikuwa katika kikosi cha Wales ambacho kilifanya maajabu kwa kufika nusu fainali ya michuano ya Euro 2016 katika mwaka ambao Leicester walichukua ubingwa.

Jeff Schlupp (Ameondoka)

Katika msimu ambao Leicester walichukua ubingwa staa huyu wa Ghana mzaliwa wa Ujerumani alicheza mechi 24. Hata hivyo, baada ya ubingwa Schlupp aliamua kuondoka zake Leicester City na sasa kwa msimu wa tatu amekuwa akikipiga Crystal Palace.

Nathan Dyer (Ameondoka)

Winga mfupi aliyekuwa msumbufu kwa mbio zake. Baada ya mafanikio ya msimu wa 2015/16. Aliamua kuondoka zake Leciester City na kutua Swansea kwa mkopo.

Hata hivyo, klabu hiyo ilishuka na mpaka sasa Dyer ameamua kubaki daraja la kwanza na klabu hiyo ya Wales.

Demarai Gray (Yupo)

Gray alijiunga na Leicester City akiwa kinda mwanzoni mwa msimu huo wa ubingwa. Kuanzia hapo ameichezea Leicester zaidi ya mechi 100 za Ligi Kuu England na sasa anaelekea kuwa mmoja kati ya wachezaji wazoefu kikosini.

Mpaka sasa yupo katika kikosi cha Kocha Brendan Rodgers akiendelea kupambania nafasi yake.

Advertisement