Kidunda aomba pambano na Mwakinyo

Muktasari:

 Kidunda alizaliwa Januari 2, 1984 mkoani Ruvuma na mwaka 2010 alishiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika New Delhi, India, na mwaka 2012 alishiriki Michezo ya Olimpiki kule London na kuchapwa na Vasile Belous raia wa Moldova  katika raundi ya kwanza.

Bondia, Seleman Kidunda ametamba kuwa atafurahi kama atatokea promota atakayewakutanisha na Hassan Mwakinyo ulingoni.

"Nimepigana mara mbili na wazawa na wote nimewashinda kwa KO katika raundi ya pili na mwezi uliopita promota, Jay Msangi alinifanyia mpango wa kupigana na bondia kutoka Afrika Kusini lakini mwisho wa siku haikufanikiwa.

"Mashabiki wangu wengi wanataka nipigane na Mwakinyo, kwangu sioni tatizo kama atatokea promota na kutupambanisha ulingoni hapo nadhani kiu yao itamalizika," alisema Kidunda.

Kidunda aliongeza kuwa  hatishwi na Mwakinyo  kwa kuwa amemfatilia katika mapambano yake na kugundua udhaifu mkubwa na endapo wakikutana ulingoni atawathibitishia wapenzi wa ngumi nani bora kati yao.

Kidunda alizaliwa Januari 2, 1984 mkoani Ruvuma na mwaka 2010 alishiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika New Delhi, India, na mwaka 2012 alishiriki Michezo ya Olimpiki kule London na kuchapwa na Vasile Belous raia wa Moldova  katika raundi ya kwanza.

Hata hivyo mwaka 2014 katika michuano ya Madola kule Glasgow, Scotland alichapwa raundi ya pili na Kehinde Ademuyiwa raia wa Nigeria  pambano ambalo waamuzi walilalamikiwa kutoa maamuzi ya upendeleo.