Kichuya,Luis kuipeleka Simba Fifa

Friday January 24 2020

Kichuya,Luis kuipeleka Simba Fifa-KLABU ya Simba -hiza Kichuya - Luis Miquissone- Ligi Kuu Bara -

 

By Mwanahiba Richard

KLABU ya Simba imesajili mawinga wawili wakati wa usajili wa dirisha dogo liliofungwa Januari 16, mwaka huu, Shiza Kichuya na Luis Miquissone ambao hadi sasa hawajacheza mechi hata moja ya Ligi Kuu Bara na wote wataendelea kusota hadi hati za uhamisho wa kimataifa ( ITC) zao zipatikane.

Hata hivyo, imebainika kuwa vyama vya soka nchini Misri na Msumbiji vinaweka ugumu kutoa ITC za wachezaji hao ambao, wamesajili dili za miaka miwili kila mmoja ndani ya Simba na hivyo kuwa watazamaji wa wenzao wanapokuwa uwanjani.

Luis yeye alianza kusajiliwa na ameshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo alicheza mechi mbili akitokea benchi huku Kichuya alisajiliwa siku ya mwisho ya kufunga dirisha la usajili.

Kwa maana hiyo, Luis ambaye alisajiliwa kutoka UD Songo ya Msumbiji alikokuwa akicheza kwa mkopo alikopelekwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, alianza mazoezi muda mrefu na Simba chini ya kocha wao Sven.

Kwa upande wake, Kichuya alianza mazoezi juzi pamoja na kikosi hicho alichokichezea msimu uliopita na kusajiliwa timu ya ENPPI ya Ligi Kuu Misri ambao, pia walimtoa kwa mkopo kwa klabu ya Pharco FC.

Hivi karibuni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema kuwa kutocheza kwa Luis ni kutokana na kuchelewa kupatikana kwa ITC na kwamba, mchakato huo unaendelea japo bado kuna ugumu.

Advertisement

Wakati wakifuatilia ITC ya Luis, Kichuya pia hataweza kuichezea Simba kwa sasa kwani, tatizo lake ni kama la Luiz kuhusu ITC kutoka Chama cha Soka nchini Misri kuweka ngumu.

Senzo alisema baada ya kuona kuna ugumu hu wa kupata ITC hizo sasa wanafikiria kuliomba Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ili kuwasaidia upatikanaji wa ITC za wachezaji hao.

“Luis na Kichuya wote wana tatizo moja ambalo ni kutopata ITC, kibali cha Luis kipo Msumbuji wakati Kichuya kipo Misri. Kuna mabishano kadhaa kwa pande za FA na klabu zao walizokuwa wakizichezea hivyo, tunataka kuiomba Fifa watupe vibali vya muda ili tuweze kuwatumia wachezaji hao wakati mengine yanaendelea.

“Hatufahamu tatizo hasa ni nini, kama ni ishu ya kimkataba ama la, ndiyo maana tunataka kwenda Fifa, ambapo pengine tutapata ufumbuzi na kujua tatizo. Kwa upande wetu tunafanyia kazi mchakato huu maana yote ni sahihi ingawa wachezaji wanachelewa kuanza kucheza,” alisema Senzo

Kwa mujibu wa taratibu za Fifa ina uwezo wa kutoa kibali kwa wachezaji ili kulinda viwango vyao endapo Simba wataandika barua kuelezea nini kinakwamisha kupatikana kwa ITC hizo kutoka klabu na vyama husika vya nchi walizokuwa wakizichezea wachezaji wao.

Hii ni kama ilivyokuwa kwa mchezaji wao wa zamani, Emmanuel Okwi raia wa Uganda alipokuwa anaichezea Etoile Du Sahel ya Tunisia alipomua kuachana nao na kwenda kucheza timu yake ya zamani ya SC Villa ya Uganda iliyomlea.

Uongozi wa Villa uliomba kibali cha muda Fifa ili Okwi aichezee timu yao kulinda kiwango chake ambapo walipewa na alipopata kibali chake ndipo aliposajiliwa Yanga ya nchini ingawa napo hakudumu kwa muda mrefu na kutimkia Simba.

Hivyo basi, Simba wakiieleza Fifa juu ya wachezaji hao huenda wakapewa vibali vya muda kwa ajili ya kulinda viwango vyao.

Tangu wasajiliwe wachezaji hao, Simba wamecheza mechi tatu za ligi ambapo Luis alikuwapo dhidi ya Yanga ingawa hakucheza na nyingine mbili za Kanda ya Ziwa dhidi ya Mbao na Alliance ambazo zote wawili hao wamezikosa.

Katika mechi hizo, Simba ilitoka sare na Yanga bao 2-2 uwanja wa Taifa, ikishinda dhidi ya Mbao bao 3-1 na Alliance FC bao 4-1 mechi hizo mbili zilichezwa ugenini uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Hivi sasa, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu wanajiandaa na mechi ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Mwadui FC itakayochezwa kesho Jumamosi uwanja wa Uhuru.

Advertisement