Kiboko ya Kichuya Yanga huyu hapa

Beki Paul Godfrey

Muktasari:

  • Chipukizi Paul Godfrey amecheza kwa mara ya kwanza mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga ambapo aliziba vyema pengo la beki Juma Abdul

Dar es Salaam. Mbabe wa mshambuliaji hodari mwenye kasi na chenga za maudhi Shiza Kichuya, beki Paul Godfrey ‘Boxer’ amegeuka lulu baada ya kumdhibiti vyema mchezaji huyo katika mchezo uliokutanisha watani wa jadi Simba na Yanga.

Godfrey, akicheza kwa mara ya kwanza mchezo mgumu wenye kila aina ya ushindani, alisimama imara kwenye nafasi ya beki wa kulia katika mchezo huo wa Jumapili ambao miamba hiyo ilitoka suluhu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kichuya ambaye mara kwa mara amekuwa mwiba mchungu kwa Yanga tangu akiwa Mtibwa Sugar, alishindwa kufurukuta baada ya kinda huyo kumpa ulinzi mkali.

Kiungo huyo wa pembeni, alishindwa kuonyesha makeke yake kabla ya kutolewa na Kocha Patrick Aussems na nafasi yake kujazwa na Mohammed Ibrahim.

Awali, mashabiki wa Yanga walihofu kuhusu uwezo wa Godfrey, baada jina la beki mkongwe Juma Abdul, kutokuwemo katika orodha kutokana na majeruhi.

Beki huyo alionyesha umahiri wa aina yake kwa kuokoa mashambulizi yaliyokuwa yakipenyezwa na viungo wa Simba, Cletus Chama na Jonas Mkude.

Simba ilitumia ujanja wa kupeleka zaidi mashambulizi kwa Godfrey wakiamini atakuwa uchochoro kwa kuwa ulikuwa mchezo wake wa kwanza mgumu tangu alipopandishwa akitokea kikosi cha pili.

Kichuya hakuwa na madhara katika mchezo huo kwa kuwa alidhibitiwa vyema na Godfrey aliyejenga ukuta imara na mabeki wengine akina Kelvin Yondani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Gadiel Michael.

Mbali na kumzuia Kichuya, mchezaji huyo alikuwa kikwazo kwa beki wa kushoto Mohammed Hussen ‘Tshabalala’ ambaye amekuwa chanzo cha mashambulizi ya Simba upande wa kushoto.

Godfrey alizuia vyema mipira ya krosi iliyokuwa ikipigwa na ‘Tshabalala’ ambaye ana sifa ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi katika mechi za Simba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Godfrey alitoboa siri ya kucheza kwa kiwango bora katika mchezo huo akidai Kocha Mwinyi Zahera, ndiye chanzo cha kufanya vyema dhidi ya wapinzani wake.

Kinda huyo alisema siku chache kabla ya mchezo, Zahera, alimwambia atampa jukumu la kucheza nafasi ya beki wa kulia kwa kuwa Abdul ni majeruhi.

“Hakuwa na maneno mengi zaidi ya kuniambia nicheze kwa kujiamini kama ambavyo nacheza katika mechi nyingine, lakini pia alinisisitiza niwe na maamuzi ya haraka kwa sababu nacheza na watu walionizidi umri na uzoefu,”alisema Godfrey.

Alisema mchezo huo ulikuwa na changamoto kubwa kwake kwa kuwa Simba ni timu bora inayoundwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye viwango bora na wengine wanatoka nje ya nchi.

Alisema mchezo huo umefungua milango ya kuongeza kasi ili kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza kwa kuwa ana safari ndefu ya kupata mafanikio katika medani ya soka.

“Nakumbuka niliingia Yanga mwaka 2016 nikitokea mtaani, nilikwenda kufanya majaribio nikapita, lakini Nsajigwa (Shadrack) aliniambia niongeze juhudi kwa sababu uwezo wa kucheza timu kubwa ninao natakiwa kuendelea kujituma, hata aliponipandisha kikosi cha kwanza aliniambia nisijione kama nimemaliza napaswa kuongeza bidii,” alisema Godfrey.

Kiwango cha Godfrey kimemuibua aliyekuwa kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula, aliyesema beki huyo anazidi kuimarika na mchezo dhidi ya Simba ulimtambulisha rasmi.

“Amepambana sana dhidi ya Simba licha ya washambuliaji wao kutaka kupitia upande wake, lakini alijitahidi kwa umri wake kutuliza mashambulizi na ukiangalia inawezekana hii ndio mechi yake kubwa ya kwanza katika ligi.

“Sijamfuatilia katika mechi nyingi lakini ana uwezo wa kucheza mpira na anajiamini, anabidi aongeze juhudi katika upigaji krosi, sio lazima mpaka aende pembeni, anatakiwa apige krosi hata akivuka upande wao, lakini kidogo kidogo anazidi kukomaa,” alisema Mwaisabula.

Naye mchambuzi wa soka Ally Mayay, alisema mchezaji huyo anatakiwa kulinda kasi yake uwanjani ili kukabiliana na kiungo hodari wa pembeni kutoka timu pinzani.

“Umri wake na kasi yake aliyonayo inaonyesha anazidi kwenda mbele kadri siku zinavyosogea, mawinga wana kasi katika mpira sehemu yoyote duniani,” alisema Mayay.

Pia Mayay amemtaka mchezaji huyo kuwa mvumilivu na kuzingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja katika kipindi chake anachocheza mpira kwa kuwa ndio nguzo muhimu katika kikosi cha Yanga.

Mchezo wa Jumapili ulikuwa wa nne kwa Godfrey katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ambapo alicheza dhidi ya Stand United, Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ na baadaye Singida Utd.