Kibadeni ampa neno zito kocha Aussems

Thursday March 14 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Kocha Patrick Aussems kutamka kuwa Simba itacheza kufa au kupona kupata ushindi dhidi ya AS Vita, baadhi ya wadau wamekosoa kauli hiyo.

Aussems akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Algeria Simba ilipokwenda kucheza na JS Saoura, alisema kuwa hatakubali kufungwa mchezo huo.

Alisema mchezo huo ni fainali kwa Simba na mkakati wake ni kushinda ili kuipa timu hiyo tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati Aussems akidai Simba itacheza kufa au kupona, kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni alisema kitendo cha kuwaaminisha wachezaji kwamba watashinda kinaweza kuwa na athari katika maandalizi.

Kibadeni alidai kitendo cha kuwaamisha wachezaji watashinda kinaweza kuwavuruga wachezaji kisaikolojia kwasababu watakwenda na matokeo.

"Timu ilikuwa kambini Zanzibar, lakini nyuma zikaundwa kamati nyingi, walianza kujiandalia sherehe mapema, walishona sare na hata wachezaji wakaaminishwa tayari wamechukua kombe kabla hata ya kucheza," alisema Kibadeni.

Advertisement

“Nina mfano halisi kuhusu mechi za namna hii, wanapojiandaa na mechi na AS Vita ni jambo jema kuwapa hamasa wachezaji lakini wasiaminishwe kuwa watashinda kabla ya kucheza,” alisema Kibadeni.

Kibadeni alikuwa kocha mkuu Simba ilipofungwa mabao 2-0 na Stella Abdjan ya Ivory Coast, katika mchezo wa fainali ya Kombe la CAF kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Dua Said alisema timu hiyo haitakiwi kujiamini itashinda mechi na AS Vita.

Nguli huyo alisema wachezaji hawapaswi kwenda uwanjani na matokeo kwa kuwa yanaweza kuwaathiri na wakacheza chini ya kiwango kama ilivyowatokea wao mwaka 1993.

Kocha wa timu ya Taifa ya Ufukweni, Boniface Pawasa alisema mchezo dhidi ya AS Vita ni mgumu kwa kuwa wapinzani wao pia nayo inategemea matokeo kwa Simba ili isonge kama ilivyo kwa Simba.

Advertisement