Khadija Kopa awakaribisha JWTZ Mwenge taarabu kwa kishindo

Muktasari:

Malkia wa taarabu nchini Tanzania,  Khadija Kopa usiku wa kuamkia juzi amenogesha uzinduzi wa bendi ya JWTZ Mwenge taarabu iliyoibuka baada ya kupotea takribani miaka 20

Dar es Salaam. Malkia wa taarabu nchini Tanzania,  Khadija Kopa usiku wa kuamkia juzi amenogesha uzinduzi wa bendi ya JWTZ Mwenge taarabu iliyoibuka baada ya kupotea takribani miaka 20.

Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na watu wa kada mbalimbali

mwanamuziki Prince Amigo na bendi ya First Class nao walionyesha uwezo wao na ilipofika saa tano usiku,  Omary Tego alipanda jukwaani sambamba na Kopa.

Kopa aligeuka kivutio kutokana na kuwafuata mashabiki waliokuwa wakisakata dansi huku akiimba wimbo wa Mjini Chuo Kikuu.

JWTZ walipanda jukwaani saa saba usiku na kabla ya kuanza kutumbuiza, walimuita Kopa kwa kile walichoeleza kuwa ni kutaka awape baraka.

“Mimi ni malkia wa mipasho wa muziki huu nawaleza  maneno haya mmerudi upya katika taarabu sasa msizembee pambaneni kwa kutoa tungo nzuri.”

“Tungo za kuweza kuwashika mashabiki na sio kutoa tungo ambazo hata hazichezeki, zimepooza  kama dagaa lisilotiwa ndimu. Mimi nawatakia baraka njema wanangu,” amesema Kopa.

Kabla ya Kopa kuteremka jukwaani, Shazy, mwanamuziki wa JWTZ alimtaka asubiri kwanza, kuanza kuimba wimbo wa Sitaki Ushambenga ulioimbwa na Omary Kopa (marehemu), ambaye ni mtoto wa Khadija.

“Nimefurahishwa kuona kijana mdogo mwenye umri sawa na  mtoto wangu akiimba namna hii na ukizingatia ameimba wimbo uliokuwa ukipendwa na mwanangu.”

“Sina la kusema nimefurahi na kukumbuka mbali sana, nikimuangalia Shazy ni kijana mdogo ameimba wimbo wa mwanangu Omary. Mungu amrehemu na ni wimbo ambao nilikuwa naupenda sana katika nyimbo zake zote.”