Kha! Ronaldo kawaacha mbali sana mishahara Italia

Wednesday September 11 2019

 

TURIN, ITALIA. SUPASTAA Cristiano Ronaldo mshahara wake wa Pauni 28 milioni anaovuna kwa mwaka huko Juventus ni mara tatu ya wachezaji wengine wanaomfuatia kwa kulipwa huko kwenye Serie A, huku akizifunika klabu zaidi ya nne kwenye bili yao ya mishahara kwa mwaka.

Ni hivi, staa huyo wa Juventus mwenye umri wa miaka 34 kwa msimu mmoja analipwa pesa nyingi kushinda klabu kadhaa kwenye Serie A mishahara yao yote inayowalipa wachezaji wao ndani ya mwaka.

Staa Ronaldo analipwa Pauni 27.7 milionni kwa mwaka, jambo hilo linamfanya azidi bili za mishahara za Klabu za SPAL, Udinese, Brescia na Verona kwenye mishahara yao zinazowalipa wachezaji wao wote ndani ya mwaka, kwamba haifiki mshahara huo wa CR7.

Juventus iliinasa huduma ya Ronaldo kutoka Real Madrid mwaka jana kwa ada ya Pauni 99 milioni.

Hata hivyo, kwenye orodha ya mishahara mikubwa Serie A, Juve ndio inayolipa kibosi zaidi.

Kwenye 10 bora, straika Romelu Lukaku ndiye mchezaji pekee asiyekuwa wa Juventus, aliyeingia kwenye orodha hiyo akilipwa mshahara wa Pauni 6.7 milioni kwa mwaka, akishika namba tatu kwa kulipwa pesa nyingi, akilingana na Gonzalo Higuain, ambapo mishahara yao ni kama theluthi moja tu ya kile anachokivuna Ronaldo kwa msimu.

Advertisement

Juve iliwanasa bure Aaron Ramsey na Adrien Rabiot, lakini inawalipa mshahara wa Pauni 6.3 milioni kwa mwaka kila mmoja, huku Paulo Dybala, anavuta Pauni 6.5 milioni.

Miralem Pjanic analipwa Pauni 5.8 milioni, akiwa juu ya Douglas Costa, Mario Mandzukic, Sami Khedira (wote Juventus), Gianluigi Donnarumma (AC Milan) na Kalidou Koulibaly (Napoli) ambao wamekuwa wakilipwa Pauni 5.4 milioni kila mmoja kwa mwaka.

Bili ya mishahara yote Juventus kwa mwaka ni Pauni 262 milioni, wakati Inter Milan ipo namba mbili kwa bili ya Pauni 124 milioni, juu ya AS Roma (Pauni 112 milioni), AC Milan (Pauni 103 milioni) na Napoli (Pauni 92 milioni).

Advertisement