Kha! Mashabiki Arsenal kweli wamemchoka Emery

Muktasari:

Sehemu kubwa ya mashabiki hao wamemtaka Emery na yeye ajiuzulu na kustaafu kuungana na David Villa, kwamba awaachie timu yao.

LONDON, ENGLAND . USIOMBEE watu wakuchoke. Mashabiki wa Arsenal wamemtaka kocha wao, Unai Emery ajiuzulu na astaafu kabisa baada kumtumia ujumbe wa kumtakia heri mchezaji David Villa, aliyetangaza kustaafu soka.

Staa huyo wa Kihispaniola alitangaza kuwa ataachana rasmi na soka mwishoni mwa msimu huu.

Na Emery ambaye alimnoa David Villa kati ya 2008 na 2010 kabla ya mchezaji huyo kwenda Barcelona, alituma meseji yake ya kumpongeza huko kwenye Twitter kwa Lugha ya Kihispaniola, jambo ambalo halikupokewa vizuri kabisa na mashabiki wa Arsenal.

Wengi waliweka komenti zao kwenye ujumbe huo wa Kocha Emery na sasa amekuwa katika wakati mgumu baada ya timu yake kushindwa kupata ushindi kwenye mechi tano mfululizo, huku mara ya mwisho kupata ushindi kwenye Ligi Kuu England ilikuwa Septemba.

Sehemu kubwa ya mashabiki hao wamemtaka Emery na yeye ajiuzulu na kustaafu kuungana na David Villa, kwamba awaachie timu yao.

Msahabiki wengi waliandika “Ondoka”, “Staafu” na “Toka” jambo lililoonyesha bayana kabisa wamemchoka kocha huyo, huku shabiki mmoja, aliandika: “Tuachie Arsenal yetu.”

Arsenal imekuwa na mwendo wa ovyo kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ambapo kwenye mechi 12 ilizocheza, imevuna pointi 17 tu na timu ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi na imefungwa mabao 17 ikiwa imefunga 16.