Kesi ya Malinzi yashindwa kuendelea, wakili mgonjwa

Muktasari:

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wako rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji wa fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria, huku wenzao Miriam na Flora wako nje kwa dhamana.

Dar es Salaam. Kesi ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Jamal Malinzi  na wenzake wanne, imeshindwa kuendelea.

Kesi hiyo ya jinai namba 213/2017 imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kile kilichoelezwa kuwa upande wa mashtaka hawana shahidi na wakili anayeendesha kesi hiyo ni mgonjwa.

Malinzi na wenzake wanakabiliwa na mashitaka 30, yakiwemo kughushi, kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha za Marekani 173, 334.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai leo alieleza hayo mbele ya hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Maira Kasonde wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili kuendelea na ushahidi.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini mimi naumwa na mpaka sasa bado naumwa, hivyo nimeshindwa kutafuta mashahidi wengine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi" alidai Swai na kuomba mahakaka ipange tarehe ufupi kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Swai baada ya kueleza hayo, hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 5, 2019 itakapoendelea na ushahidi.

Mbali na Malinzi, washitakiwa wengine ni aliyekuwa  Katibu Mkuu wa TFF,  Selestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Meneja wa TFF Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya.

Tayari mashahidi 15 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi dhidi ya Malinzi akiwemo aliyekuwa dereva wake.

Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao ni aliyekuwa Mkaguzi  wa ndani wa Kampuni ya Bia Tanzania(TBL), Richard Magongo, ambaye alidai kuwa  waliingia mkataba wa kuwadhamini Taifa Stars kwa miaka mitano kwa jumla ya Dola  za Marekani 10,000,000.

Shahidi huyo, alidai akiwa mkaguzi wa ndani baadhi ya fedha zilizotolewa na TBL kwa Shirikisho la mpira wa miguu(TFF) kwa ajili ya udhamini wa timu ya Taifa Stars zilitumika bila kuwa na nyaraka za uthibitisho wa matumizi.

Magongo, alidai baada ya kuingia mkataba na TFF wa udhamini wa Taifa Stars mwaka 2012 kwa kipindi cha miaka mitano walikuwa wanafanya ukaguzi wa fedha hizo kila robo mwaka.

Shahidi huyo alidai baada ya ukaguzi huo alibaini kwamba fedha za udhamini zilitumika bila kuwa na nyaraka za uthibitisho wa matumizi.

Hata hivyo, Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wako rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji wa fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria, huku wenzao Miriam na Flora wako nje kwa dhamana.