Kerr wa Gor Mahia aanza kuchonga

Tuesday June 26 2018

 

By THOMAS MATIKO

KOCHA wa Gor Mahia, Mwingereza Dylan Kerr kadai kuwa kikosi chake wala hakiwaziii ubingwa wa ligi kuu  ya KPL kwa sasa, licha yao kuwa kwenye fomu hatari.

Mpaka sasa ikiwa ni baada ya kupiga mechi 17 za ligi kuu huku wakiwa na tatu kibindoni ili kufikisha idadi sawia na timu zinginezo ligini, Gor wamejikuta kileleni kwa jumla ya alama 43.

Mpinzani wake wa karibu kwa mara nyingine tena kama tu msimu uliopita akionekana kuwa Sofapaka,  yupo nyuma kwenye nafasi ya pili kwa alama 34, akiachwa na pointi tisa zaidi.

Hadi kufikia sasa  Gor hajapoteza mechi hata moja huku akitoka sare nne pekee. Anaongoza kwa ufungaji magoli akiwa amecheka na nyavu mara 40 huku akifungwa mabao 15.

Kwa takwimu hizi tayari wachanganuzi wameshampa Gor ubingwa. Awali wengi walidhania utakuwa mtihani mgumu kutokana na mashindani kibao anayoshiriki Gor ikiwemo ile ya Barani CAF Confederation, GOTV Shield Cup  ila Gor wameonyesha kiwang licha ya presha ya mechi nyingi.

Na sasa mambo kwenye ligi  yakionekana kuwaendea kama wanavyotaka, kocha Kerr kadai kuwa ni mapema sana na kwamba mawazo yao wala hayapo kwenye ubingwa muda huu.

“Hatuwezi kupumzika. Tumempiga Ulinzi Stars na kupanua mwanya kwa alama tisa, hiyo kwetu ni historia sasa tuaangalia mbele. Kisaikolojia hii ni hali nzuri sana kwetu lakini hatuwezi kuwa na mawazo ya taji kwa sasa” amesema Kerr.

Advertisement