Kelvin John 'Mbappe' mbona kucheza Ulaya sio tatizo

Muktasari:

Kuelekea fainali hizo cha Chan, Mwanaspoti imefanya mahojiano na kinda huyo ambaye amefunguka makubwa anayotarajia katika mashindano hayo na maisha yake ya soka kwa ujumla.

UKIACHA Mbwana Samatta, matumaini makubwa ya Watanzania kuona nyota wao wakitoboa kiukweli ukweli katika soka la kimataifa yapo kwa kinda mwenye kipaji cha kipekee nchini, Kelvin John ‘Mbappe’.

Katika umri wake wa miaka 17 tu, tayari Kelvin ni gumzo kila kona nchini.

Baada ya kutisha katika majaribio aliyoenda kufanya katika academy ya Ajax Amsterdam nchini Afrika Kusini, kikwazo pekee kwa Kelvin kuvamia soko la kimataifa linalojali sana wachezaji wenye umri mdogo, ni sheria kali za FIFA zinazodhibiti vijana wa umri chini ya miaka 18 kuuzwa nje ya nchi zao. Matarajio makubwa juu ya kipaji cha Kelvin yalionyeshwa pia na gwiji wa soka Afrika na Ulaya, Emmanuel Amunike, aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambaye alimuita katika kikosi cha wachezaji 45 kwa ajili ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019.

Jina lake liliendelea kuwapo kikosini hadi lilipoondolewa katika mchujo wa mwisho uliobakisha nyota 23 ambao walioiwakilisha nchi katika mashindano hayo nchini Misri.

Kelvin ameendelea kuaminiwa na mrithi wa Amunike baada ya Tanzania kutolewa katika makundi ya AFCON, Etienne Ndayiragije, ambaye anakaimu nafasi ya kocha mkuu wa Stars akisaidiana na Juma Mgunda na Selemani Matola.

Ndayiragije amemuita Kelvin katika kikosi chake cha wachezaji 26 kinachojiandaa kuivaa Kenya katika michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani Julai 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kuelekea fainali hizo cha Chan, Mwanaspoti imefanya mahojiano na kinda huyo ambaye amefunguka makubwa anayotarajia katika mashindano hayo na maisha yake ya soka kwa ujumla.

KUITWA STARS

“Nilijisikia faraja sana kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa. Licha ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza, lakini nimeandika historia ya kuitwa nikiwa na umri mdogo katika kikosi ambacho kimesheheni wakongwe na wazoefu wa ligi.

“Nimerudishwa tena baada ya kuchujwa katika mchujo wa kocha Amunike, nafikiri endapo nitapewa nafasi ya kucheza nitakuwa nimeandika rekodi nyingine na nitatumia nafasi hiyo kufanya kitu kikubwa zaidi ili kuendelea kuwapa imani makocha wanaoniamini,” anasema.

“Nafurahi kuona kile ninachokifanya kinatambuliwa. Nafurahi kuwa miongoni mwa Watanzania wachache ambao wanatarajia kuiwakilisha nchi katika fainali za Chan, malengo ni kufanya vizuri, hatutawaangusha Watanzania. Wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti hiyo Julai 28,” anasema.

TANO LA SAMATTA

Anasema nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alimpongeza kuitwa kwake akiwa na umri mdogo katika kikosi cha timu ya taifa na kumtaka aendelee kupambana ili kufikia mafanikio na hatimaye aweze kuwa mchezaji tegemeo kikosini kwa miaka ya baadaye.

“Ilikuwa ndio siku yangu ya kwanza kuonana na Samatta uso kwa uso, nilijisikia vizuri, lakini mbali na kufurahia kumuona, kikubwa alichoniambia amefurahi kuona naitwa kikosini nikiwa na umri mdogo na kunitaka kutoridhika na hilo, bali niendelee kupambana,” anasema.

KUIKOSA AFCON

“Nilifurahi kuwa miongoni mwa nyota waliojumuishwa kikosini. Suala la kukosa nafasi yay a kwenda AFCON halikuvuruga furaha yangu kwani nilijifunza vitu vingi kutoka katika maandalizi ya mashindano hayo sambamba na kuamini katika kujituma.

“Nimekutana na wachezaji wengi walionitangulia katika sok,a nimefundishwa kujituma na kuamini kuwa naweza, hivyo nimefurahia hilo na wala sijachukizwa kukosa kucheza mchezo hata mmoja. Kuna wengine hawakupata hata bahati ya kuitwa na katika Biblia kuna maneno yanasema shukuru kwa kila jambo,” anasema.

MALENGO YAKE

“Mimi maisha yangu ni mpira hivyo nategemea kupata mafanikio kupitia soka. Kikubwa ninachomuomba Mungu ni kuniepusha na matatizo yanayotokana na mpira, aidha kwa kuvunjika au kusimamishwa kujihusisha na soka kwasababu malengo yangu ni kupambana kucheza soka vizuri ili niweze kucheza Ulaya,”

“Hakuna mchezaji mwenye malengo ya kuendelea kubaki Tanzania. Kila mmoja anatamani kufika mbali zaidi kwa kucheza soka la kulipwa, hivyo kutokana na changamoto hiyo ili niweze kuifikia ndoto yangu ninahakikisha napambana na kutokukubali kukatishwa tamaa na kuamini nina uwezo na ninaweza kufika ninapopataka,” anasema.

SIKU MOJA KABLA YA MECHI

Anasema wakiwa na mchezo wowote, siku moja kabla wamekuwa wakikutana timu nzima na kujadili mbinu za kuwakabili wapinzani wao na kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakifanikiwa na ndio siri ya wao kupata matokeo mazuri.

“Mbali na kikao cha pamoja na benchi la ufundi sisi kama wachezaji huwa tunakaa pamoja. Kama timu ni mpya hatujawahi kukutana nayo, tunajadili namna na muda wa kuwasoma wapinzani na kama timu tunaijua, tunapangiana majukumu kila mmoja nani anafanya nini na nani anamkaba yupi,” anasema.

JEZI NAMBA 10

Wachezaji huchagua namba za jezi zao mgongoni kutokana na sababu mbalimbali na kwa Kelvin hali ni hiyo hiyo.

“Navaa jezi namba 10 kwasababu ndio tarehe yangu ya kuzaliwa. Huwa naitumia kama kumbukumbu. Niliamua kuchagua tarehe na sio mwezi kwasababu kwa upande wa mama yangu lilikuwa ni tukio zuri kunipata mimi katika tarehe hiyo,” anasema.