Kazi nzuri yampa Herrera dili jipya

Muktasari:

Mkataba wa sasa wa Herrera utafika tamati mwishoni mwa msimu, lakini kinachoelezwa ni kwamba dili hilo jipya atakalosaini halitakuwa na mabadiliko kwenye mambo ya mshahara, ataendelea kulipwa kwa kiwango kilekile cha Pauni 100,000 kwa wiki.

MANCHESTER, ENGLAND . KAZI nzuri inalipa unaambiwa. Ander Harrera kwa sasa anasubiri tu dili matata kabisa litakalomfanya aendelee kubaki kwenye kikosi cha Manchester United kwa muda mrefu.

Kinachoelezwa ni kwamba staa huyo Mhispaniola anaweza kusaini dili jipya la miaka mitatu la kuendelea kubaki Old Trafford hasa baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa kwa sasa tangu Kocha Ole Gunnar Solskjaer alipotua kuchukua mikoba ya Jose Mourinho.

Kipindi cha Mourinho mchezaji huyo alikuwa akipiga hesabu za kuondoka, lakini kwa sasa mambo yamekaa vyema, huku akiwa mchezaji muhimu kabisa katika safu ya kiungo ya timu hiyo.

Mkataba wa sasa wa Herrera utafika tamati mwishoni mwa msimu, lakini kinachoelezwa ni kwamba dili hilo jipya atakalosaini halitakuwa na mabadiliko kwenye mambo ya mshahara, ataendelea kulipwa kwa kiwango kilekile cha Pauni 100,000 kwa wiki.

Chanzo cha kutoka Old Trafford kilifichua: “Ander yupo tayari kubaki na mambo sasa yameonekana kutulia. Klabu imemweleza wazi inamtaka abaki, hawataki aondoke bure. Familia yake pia imetulizana Manchester na mwenyewe amekuwa maarufu sana kwa mashabiki.”

Herrera amekuwa akifuatiliwa na klabu kibao za Ulaya ikiwamo timu yake ya zamani ya Athletic Bilbao.

Hivi karibuni, Man United imewasainisha mikataba mipya wachezaji Anthony Martial, Phil Jones, Chris Smalling na Ashley Young huku kipa David De Gea akiwa kwenye hatua za mwisho kukubaliana na timu kusaini dili litakalomfanya awe analipwa Pauni 350,000 kwa wiki na kuwa kipa anayelipwa pesa nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England.