Katwila atoa siku tatu Mtibwa Sugar

Muktasari:

Mtibwa Sugar ni bingwa wa Ligi Kuu Bara katika misimu miwili mwaka 1999 na mwaka 2000.

IKIWA Ligi Kuu Bara imesimama kutokana na ugonjwa wa corona, kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amewapa wachezaji wake siku tatu.

Katwila ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20, alisema kutokana na ligi kusimama amewapa wachezaji wake programu maalumu.

Anasema amewapa programu ya kila siku ya wiki kufanya mazoezi ambayo kila siku yanakuwa na utofauti.

"Kuanzia Jumatatu mpaka Jumapili kuna mazoezi ya tofauti ambayo kila mchezaji anatakiwa kuchukua siku tatu kati ya saba za wiki kufanya mazoezi.

"Nimetoa programu ya wiki nzima lakini nimewaeleza wachezaji wangu wanatakiwa kuchukua hata siku tatu kila mmoja kufanya mazoezi hayo.

"Kama kuna ambaye atapenda kufanya mazoezi yote ya wiki nzima itakuwa jambo jema kutokana anaweza kuimarika zaidi," alisema.

"Nafahamu wachezaji wa Kitanzania walivyo ni ngumu kufanya mazoezi akiwa mwenyewe ndio maana nimewataka walau siku tatu wafanye hiyo ratiba ambayo nimewapa ya wiki nzima," alisema Katwila.

"Nimekuwa nikiwafuatilia wachezaji wangu kuanzia kundi letu la timu (Whatsapp Group), ambalo tumekuwa tukipeana ratiba ya kila siku na mambo mengine ya kufanya," aliongezea Katwila.

Katwila alisema kusimama kwa ligi si kwamba ikija kuanza watapewa ratiba ya kushtukiza bali watapewa muda wa kujiandaa kama timu.

"Nadhani si kwamba tutaanza tu ligi kwa mazoezi haya binafsi ya wachezaji bali tutapata muda wa kutosha kama timu kufanya mazoezi ya pamoja.

"Kama ikiwa tofauti na hivyo halitakuwa jambo sahihi kwetu linaweza kutuumiza kutokana na aina ya wachezaji ambao tunao," alisema Katwila.