Katwiga FC inakuja Kombe la FA Mwanza

Muktasari:

Ulikuwa mchezo wa fainali ya kumsaka mshindi atakayefuzu Hatua ya Ngazi ya Mkoa ya Kombe la Shirikisho ambapo Katwiga imefanikiwa kufuzu baada ya ushindi huo.

MWANZA. KATWIGA FC imefanikiwa kufuzu hatua ya pili ngazi ya Mkoa wa Mwanza kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuilaza Kaseni mabao 3-2 katika mchezo uliopigwa juzi katika Uwanja wa Nyamagana.

Mchezo huo ambao ulikuwa wa fainali kumsaka bingwa ambaye ataungana na Phantom FC kucheza ngazi ya Mkoa, ilishuhudiwa patashika kwa timu zote kuonyesha uwezo wa hali ya juu.

Licha ya Kaseni kutangulia kupata mabao yao mawili,Katwiga waliwaduwaza wadau wa soka waliojitokeza uwanjani hapo kwa kutoka nyuma na kusawazisha mabao yote na kufunga la ushindi.

Kaseni walianza kuandika bao dakika ya 33 kupitia kwa Juma Mussa kisha Joseph John akaiandikia la pili dakika ya 66 mabao ambayo yalianza kusawazishwa dakika ya 77 kupitia kwa Lucas Daud.

Kama haitoshi Katwiga iliweza kupata bao la pili lililofungwa na Daniel Ndalo dakika ya 85 na kabla ya kipyenga cha mwisho Daud akaiongezea bao la tatu lililoivusha hatua hiyo na kusonga mbele.

Kocha wa katwiga FC,Hamis Gidion alisema kuwa kwa sasa wanaenda kujipanga na hatua ya inayofuata na kutamba kuwa wamejipanga kuwashangaza wengi katika michuano hiyo.

Alisema kuwa wanaamini watapata ushindani katika hatua inayofuata jambo ambalo litawajenga wachezaji kujiamini na kwamba matarajio yao ni kufika mbali.

“Kwanza tunashukuru Mungu kwa kuweza kufuzu hatua hii,tunajua huko mbeleni kuna ushindani kwa sababu tunaenda kucheza na timu kubwa,lakini tumejiandaa na tutashangaza wengi”alitamba Kocha huyo.