Katika Ligi Daraja la Kwanza vita imekolea

Muktasari:

Kundi A linaloongozwa na Dodoma FC yenye alama 48 sawa na Ihefu FC inasaka ushindi ambao utawafanya kubaki kileleni ili kucheza Ligi Kuu itakapovaana na Iringa United inayokwepa kushuka daraja.

HATMA ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) itajulikana wikiendi hii inapohitimishwa huku timu moja ya Kundi A ndio itakayopata tiketi ya kupanda Ligi Kuu moja kwa moja na nyingine kuingia hatua ya mtoano.

Kundi A linaloongozwa na Dodoma FC yenye alama 48 sawa na Ihefu FC inasaka ushindi ambao utawafanya kubaki kileleni ili kucheza Ligi Kuu itakapovaana na Iringa United inayokwepa kushuka daraja.

Ihefu FC itaikaribisha Cosmopolitan kwenye Uwanja wa Highland Estates ambayo tayari imeshuka daraja.

Kocha wa Ihefu FC, Maka Mwalwisi anasema hawana kitu cha kupoteza kwenye mchezo huo sababu bado wanayo nafasi ya kupambana hadi hatua ya mwisho kupingania nafasi ya kwanza. “Kwenye soka lolote linaweza likatokea, kila timu inayonafasi ya kushinda, hivyo tukipata alama tatu halafu Dodoma wakaambulia sare ina maana tumepita na kupanda Ligi Kuu,” alisema Mwalwisi.

Hata hivyo, Mbwana Makata kocha wa Dodoma anasema michezo yote wanacheza kama fainali kwa kutambua ushindani ulivyo kwenye kundi lao.

“Tunatambua nafasi tuliyokuwa nayo na kiu ambayo watu wa Dodoma wanavyoitarajia, kikubwa ni kupambana bila kujali tunacheza na timu ya aina gani,” alisema Makaka.

Geita Gold tayari imejikatia nafasi ya kucheza hatua ya mtoano huku Gipco FC, Transit Camp, Rhino Rangers na AFC wakiwania nafasi moja iliyosalia kwa upande wa Kundi B.

Kundi A, Dodoma na Ihefu mmoja atasalia nafasi ya kucheza hatua ya mtoano, huku Majimaji na Mbeya Kwanza wakipambania nafasi nyingine iliyobaki.

Mlale FC, Pan African, na Cosmopolitan tayari wameshaaga ligi hiyo huku, Green Warriors na Sahare All Stars kutoka Kund B nao wameshuka hata kabla ya michezo ya wikiendi hii.

Michezo mingine ya wikiendi hii Njombe Mji atacheza na Mbeya Kwanza, Boma FC dhidi ya Friends Rangers, Pan African na Majimaji, African Lyon akivaana na Mlale FC, Gwambina FC itacheza na Mashujaa, Pamba FC Rhino Rangers, Mawenzi na Stand United, Geita Goldna Transit Camp wakati Gipco na Green Warriors.