Katibu mkuu mpya Yanga huyu hapa

Muktasari:

  • Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema mabosi wa Jangwani tayari mezani kwao kuna majina matatu moja la aliyekuwa mtendaji mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba na jingine la aliyekuwa pia meneja wa klabu hiyo ya Chamazi, Jemedari Said bosi mmoja wa benki naye inaelezwa kuwa mmojawao ndiye anayeweza kumrithi Mkwasa.

WAKATI kambi ya Yanga mjini Morogoro ikizidi kunoga kwa nyota wapya na wale wa zamani wakianza kuonyesha kuzoeana mazoezini, unaambiwa mabosi wa klabu hiyo wapo hatua ya mwisho kumtangaza katibu mkuu mpya, huku majina matatu yakitajwa.

Yanga iliyopata viongozi wapya kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mapema Mei mwaka huu, kwa sasa inahaha kuunda sekretarieti mpya, lakini majina mawili yakitajwa juu ya kuchukua nafasi ya ukatibu mkuu iliyokuwa ikishikiliwa na Charles Boniface Mkwasa.

Kwa muda nafasi hiyo tangu Mkwasa alipojiuzulu ilikuwa ikikaimiwa na Omar Kaya ambaye muda wake ulishamalizika na kukabidhiwa kwa muda mfupi kwa ofisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten.

Hata hivyo, Ten naye mkataba wake wa kufanya kazi Yanga umeshaisha mchana wa jana wakati mchakato wa kupata katibu mkuu wa kushika nafasi hiyo ukiwa kwenye mstari baada ya klabu hiyo kutangaza nafasi za kazi ikiwamo hiyo ikielezwa kila kitu kipo safi.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema mabosi wa Jangwani tayari mezani kwao kuna majina matatu moja la aliyekuwa mtendaji mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba na jingine la aliyekuwa pia meneja wa klabu hiyo ya Chamazi, Jemedari Said bosi mmoja wa benki naye inaelezwa kuwa mmojawao ndiye anayeweza kumrithi Mkwasa.

Kawemba aliyewahi kuwa bosi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), anapigiwa hesabu hizo kutokana na uzoefu wake katika majukumu ya mpira, huku mpinzani wake ambaye ni nyota wa zamani wa soka naye akitajwa kuwa na mafanikio makubwa kisoka.

Mbali na kucheza kwa kiwango cha juu na kuwa mzoefu wa masuala la uongozi kwani chini ya uongozi wake Azam ilibeba taji la Ligi Kuu Bara, pia ni meneja wa nyota kadhaa wa soka nchini akikubalika zaidi kwa baadhi ya vigogo wa klabu hiyo ya Jangwani.

Licha ya Mwanaspoti kuutafuta uongozi wa klabu hiyo akiwamo Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla ili ufafanue juu ya taarifa hizo, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa kwa muda mrefu siku ya jana.