Kaseke: Simba ilistahili kimataifa

Muktasari:

Simba tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na imebakiwa na mechi mbili tu kumaliza msimu.



WINGA wa Yanga, Deus Kaseke amesema kiufundi Simba imestahili kucheza kimataifa, akitoa sababu kwamba ilipambana kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ikafikia lengo lake.

Kaseke alisema asiyekubali kushindwa sio mshindi, aliifafanua kauli hiyo kuwa timu 20 ambazo zilicheza ligi msimu huu, zilikuwa zinasaka taji ambalo Simba imeshinda na imepata, hivyo anaona inastahili nafasi hiyo.

“Simba ilikuwa kwenye kiwango ambacho kimewabeba kuchukua ubingwa, sina maana sisi hatukujituma, ila ushindani ndivyo ulivyo huenda na msimu ujao tukawa katika kiwango kingine cha juu,” alisema.

Mbali na kuiona Simba inastahili kwenda kimataifa, pia aliweka wazi kitu ambacho kimemfurahisha kwa msimu huu kwamba, amecheza kwenye kiwango ambacho alikuwa anakitaka kwa muda mrefu sasa.

“Nilitamani kucheza kwa kiwango hicho ambacho nimeonyesha katika msimu huu, ingawa hakitanifanya niridhike kwani najipanga kuhakikisha kila msimu nakuwa na hatua zaidi ya uliopita,” alisema.