Kaseja aachwa Kilimanjaro Stars, Manula kuongoza jeshi Uganda

Muktasari:

Kilimanjaro Stars ipo Kundi B lenye timu za Kenya, Sudan na Zanzibar wakati Kundi A linaundwa na wenyeji Uganda, Burundi, Djibout, Eritrea, Somalia katika mashindano hayo.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda amemwacha kipa Juma Kaseja na kumchukua Aish Manula katika kikosi chake cha wachezaji 22 watakaocheza mashindano ya Kombe la Chalenji Cecafa yatakayoaanza mwishoni mwa wiki hii.

Kilimanjaro Stars inaondoka leo Alhamisi ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri katika Kundi B lenye timu za Kenya, Sudan na Zanzibar wakati Kundi A linaundwa na wenyeji Uganda, Burundi, Djibout, Eritrea, Somalia katika mashindano hayo.

Katika kikosi chake nahodha msaidizi Juma Kaseja ameachwa katika kikosi hicho na nafasi yake ikichukuliwa na kipa Manula.

Manula aliachwa katika kikosi hicho tangu kumalizika kwa fainali za Mataifa ya Afrika Afcon2019, Misri na nafasi yake kuchukuliwa na Kaseja jambo lililozua gumzo kubwa.

Kaseja ameidakia Tanzania na kuisaidia kufuzu kwa CHAN2020, Cameroon pamoja na kufuzu kwa hatua ya makundi ya kusaka nafasi ya kucheza Kombe la Dunia 2022 Qatar.

Mgunda aliwahita Manula na Kaseja katika kikosi chake cha awali kilichokuwa na wachezaji 30, lakini leo katika kikosi cha mwisho jina la Kaseja halimo hiyo ni wazi ametoa nafasi kwa Manula.

Akizungumza wakati wa kutangaza kikosi hicho Mgunda alisema wachezaji wake wapo katika hali nzuri baada ya mazoezi ya leo asubuhi na watakaoachwa ni kutokana na sababu mbalimbali za kiafya na mambo mengine ya kiufundi.

"Watanzania watarajie mambo mazuri kutoka kwa vijana wao, tunakwenda kupambana tukiwa na wachezaji waliojaa morali ya hali ya juu, siku zote tunakuwa watu wa kupambana, tunaahidi kufanya vyema," alisema Mgunda.

Hata hivyo hakuweza kuweka wazi wachezaji watakaoachwa zaidi ya Salum Kimenya anayesumbuliwa na malaria, Salum Abubakari 'Sure Boy', Idi Seleman "nado", Shaaban Idd Chilunda na Frank Domayo wanaosumbuliwa na matatizo ya kiafya.

"Ripoti kamili ya majina ya wachezaji watakaokwenda na wale watakaobaki itatolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) muda mfupi kabla ya timu kuondoka kwenda Uganda."

Wachezaji 22 wanaondoka ni, Metacha Mnata (Yanga), Aishi Manura (Simba), David Kisu (Gor Mahia), Juma Abdul (Yanga), Nickson Kibabage (Difaa El Jadida), Gadiel Michael (Simba), Mwaita Gereza ( Kagera), Mohamed Hussein (Simba), Kelevin Yondani (Yanga), Bakari Mwamnyeto (Coastal Union) na Baraka Majogoro (Polisi Tanzania).

Wengine, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga (wote Simba), Zawadi Mauya (Kagera), Ditram Nchimbi (Polisi Tanzania), Mkandala Cleoface (Prisons), Miraji Athuman (Simba), Eliuter Mpepo (Buildcon-Zambia), Lukasi Kikoti (Namungo) na Rashid Chombo (IK Frej Taby- Sweden)