Kaseja, Kagere ndani ya kikosi bora kufuzu Kombe la Dunia Afrika

Muktasari:

Timu 14 zilizofanya vizuri kwenye hatua ya awali ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwak 2022 huko Qatar, zitaungana na nyingine 26 zilizovuka hatua hiyo moja kwa moja, kufanya jumla ya timu 40 nambazo zitagawanywa kwenye makundi 10 yatakayotoa washindi 10 ambao watacheza mtoano kusaka nchi tano (5) zitakazotinga Qatar.

Dar es Salaam.Hatua ya awali ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 huko Qatar kwa upande wa Bara la Afrika, imekamilika jana Jumanne kwa michezo 10 ya marudiano kuchezwa katika maeneo tofauti barani humu.

Kiujumla mechi hizo za hatua ya awali zilishirikisha jumla ya nchi 28 ambazo zipo chini kwenye chati ya viwango vya ubora wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa upande wa Kanda ya Afrika.

Matokeo na matukio ya kushangaza yalijitokeza kwenye baadhi ya mechi hizo 14 za marudiano huku ushindani wa hali ya juu ukioneshwa na wachezaji wa timu mbalimbali.

Wapo wachezaji waliofanya vyema na kuzibeba nchi zao kwenye mechi hizo za marudiano hadi zikaweza kutinga hatua inayofuata ya mashindano hayo, lakini wapo ambao walichemsha na kushindwa kuwa na msaada kwa mataifa yao.

Makala hii inakuletea tathmini ya wachezaji 11 ambao walionyesha kiwango kizuri na kuzisaidia timu zao na kutokana na kile walichokifanya wanaunda kikosi bora cha mechi za marudiano za kuwania kutinga hatua ya makundi ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022.

1.  Kaseja Juma –Tanzania

Aliweka hai matumaini ya Taifa Stars katika mechi ya marudiano dhidi ya Burundi kwa kuokoa mashambulizi mawili ya ana kwa ana yaliyofanywa na wapinzani wao kupitia kwa Saido Berahino na Bimenyimana Bonfilscaleb ambayo yangeweza kuipatia Burundi, mabao ambayo yangeifanya Tanzania iage mashindano hayo.

Pamoja na kuilinda sare ya bao 1-1 iliyopatikana kwenye dakika 120 za mchezo kwa kuokoa mashambulizi hayo mawili hatari, Kaseja aliokoa moja ya penalti tatu za Burundi na kuiwezesha Stars kuibuka na ushindi wa mikwaju 3-0 ya penalti.

2. Isaac Correia- Angola

Alikuwa kwenye kiwango bora kwenye mechi ya nchi yake dhidi ya Gambia ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kufanikiwa kufuzu hatua inayofuata kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1.

Alipandisha vyema mashambulizi na kufanya vizuri kwenye ulinzi na ndiye alipiga pasi iliyozaa bao la pili lililofungwa na Fabio Gooncalves Abreu dakika ya 68.

3.  Divine Lunga-Zimbabwe

Katika mchezo uliokuwa wa presha kubwa kwa wenyeji Zimbabwe dhidi ya Somalia, Lunga anayechezea Golden Arrows ya Afrika Kusini alikuwa mwiba kwa wapinzani kutoikana na jinsi alivyokuwa  akipandisha mashambulizi kutokea upande wa kushoto jambo lililolazimisha winga na beki wa kulia wa Somaliza wakae nyuma muda karibia wote wa mechi.

4.  Alvin MCCONNEL-  Liberia

Baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Sierra Leone, Liberia ilihitaji, ushindi au sare ya aina yoyote ama kutopoteza mechi kwa kipigo cha zaidi ya mabao 2-0 ugenini ili isonge mbele na ndicho kilichokuja kutokea kwani ilichapwa bao 1-0 na kufuzu hatua ya makundi.

Hata hivyo hakuna namna ambayo Liberia wanaweza kujivunia kufuzu bila kumpa sifa za ziada beki wao wa kati, Alvin McConnel ambaye aliweka hai matumaini yao kwa kufanya kazi nzuri ya kuokoa mpira uliopigwa na nyota wa Sierra Leone, Kei Kamara ambao ulikuwa unaelekea nyavuni baada ya kipa wake kutoka vibaya.

5.  Frederic NSABIYUMVA- Burundi

Pamoja na Burundi kuondolewa na Taifa Stars, beki wake Fredric Nsabiyumva anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini kwenye klabu ya Chippa United alionyesha kiwango bora kwa kuwadhibiti washambuliaji wenye uchu wa Tanzania ambao walilishambulia lango la Burundi mara kwa mara na matokeo yake walipachika bao moja tu tena lililotokana na mpira wa kona.

6. Mukunzi Yannick- Rwanda

Aliilinda vyema safu ya ulinzi ya Rwanda kuichezesha na kuiunganisha vyema timu dhidi ya Shelisheli na kuiwezesha nchi yake kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Shelisheli na pamoja na kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, aliweza kufunga moja kati ya mabao hayo.

7. Admiral Muskwe- Zimbabwe

Aliingia akitokea benchi huku timu yake ikiwa haijafunga bao, lakini alifanya kile kilichotegemewa na wengi kwa kufunga bao moja na kutoa pasi ya bao la tatu lililofungwa na Khama Billiat ambalo liliiwezesha nchi yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ulioipeleka hatua ya makundi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

8. Shimelis Bekele-Ethiopia

Ethiopia ilihitaji ushindi au sare ya mabao ugenini dhidi ya Lesotho ili isonge mbele kwenda hatua inayofuata baada ya timu hizo kutoka sare tasa kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika huko Addis Ababa

Walifanikiwa kutoka sare ya bao 1-1, lakini kazi kubwa ilifanywa na nahodha wao Shimelis Bekele ambaye alitibua mipango ya wenyeji ambao walilazimika kutojilipua na kushambulia kila wakati ili kumchunga nyota huyo anayechezea klabu ya Masr el Makasa.

9. Kagere Meddie-Rwanda

Alipachika mabao mawili ambayo yalikuwa miongoni mwa saba ambayo Rwanda iliyapata kwenye mechi yake ya marudiano nyumbani dhidi ya Shelisheli

10. Tuyisenge Jacques-Rwanda

Alikitendea haki kitambaa cha unahodha cha Rwanda kwa kutengeneza nafasi, kupiga pasi za mwisho na pia kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 7-0 ambao ulikuwa ni mkubwa zaidi kuwepo katika mechi za hatua ya awali ya kufuzu Kombe la Dunia kwa Kanda ya Afrika.

11. Khama Billiat-Zimbabwe

Alikuwa mwiba kwa mabeki wa Somalia kutokana na chenga, uwezo wa kumiliki mpira, chenga na kasi jambo lililopelekea afanyiwe madhambi mara kwa mara na kama jaitoshi ndiye alifunga bao lililoivusha Zimbabwe kenda hatua inayofuata.