Karia: Mimi ni Simba, ila ukweli upo hivi!

ZILE kelele za mashabiki wa soka juu ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba umejaa unazi wa Simba kiasi cha kushindwa kuficha mahaba yake, limemfanya Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia kuvunja ukimya kwa kuwajibu wale wanaousakama uongozi wao.

Kelele zaidi zimekuja kutokana na sakata la winga Mghana Bernard Morrison na mzozo wake dhidi ya klabu yake ya zamani, Yanga na ule uamuzi wa kumuidhinisha winga huyo kujiunga na kuichezea Simba, lakini Karia amekiri ni kweli kwa muda mrefu amekuwa akisikia malalamiko hayo dhidi yao na kusema;

“Nimesikia hizo tuhuma, ila ukweli huko hivi, mimi ni kiongozi wa soka, sio wa klabu ya Simba, hata kama ikitokea naipenda Simba, lakini kwenye haki nitasimamia haki.”

Karia, alisema ameyasikia madai hayo na watu kumshambulia kwenye mitandao, lakini uongozi ndivyo ulivyo.

“Siwezi kuacha kutenda haki kwa sababu ya Simba au Yanga, hilo kwenye uongozi wangu halipo, wanaonihusisha kuipenda Simba na kuwa shabiki kindakindaki, wacha waseme, lakini ukweli wa utendaji wangu haugemei upande wowote.

“Simba ikikosea itaadhibiwa kwa mujibu wa kanuni, vivyo hivyo Yanga na klabu nyingine, mimi ni muumini wa haki, napenda haki na huwa siku zote nataka hatua zichukuliwe bila kupepesa macho.”

Alisema katika uongozi wake, hayupo kwa ajili ya timu fulani, anaongoza soka na ni kiongozi wa klabu zote.

“Nimewasikia watu wanazungumzia kuhusu mimi kuipenda Simba, wengine wanasema naipendelea, siwakatazi kuzungumza huko kwenye mitandao, ila kama yupo mwenye ushahidi, aje tukutane uso kwa uso anithibitishie hilo,” alisema.