Kapuya: Mlitaka nioe bibi?

Muktasari:

Kapuya amesema kwa mara ya kwanza amekutana na Mwajuma Kaliua, alipokuwa anaenda kufanyia vikao na Kaliua na Urambo sio mbali.

Profesa Juma Kapuya aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Magharibi,amefunguka kuhusu ndoa yake aliyofunga Jumapili ya  Februari 12 na mwanamke anayejulikana kwa jina la Mwajuma Mwiniko.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kapuya amesema anawashangaa watu wanaomsema kuoa mwanamke aliyemzidi umri kwani wanataka aoe mwanamke anayefanana na bibi yake?
Kapuya amesema umri hauhusiani na mapenzi, hivyo watu wakubali matokeo kwani hajamtorosha shule huyo mwanamke,wala hajavunja sheria, mila, desturi pamoja na dini.
"Unajua mimi nawashangaa sana watu wanaoshangaa mimi kuoa mwanamke niliyemzidi umri,hivi umri unahusiana nini na mapenzi? Na ukiangalia huyu mwanamke mimi sijamtorosha shule, wala sijavunja mila, desturi pamoja na dini, au watu walitaka nioe mwanamke anayefanana na bibi yangu? Nawaambia wakubali matokeo tu waache kusema sema," alisema Kapuya.
Aidha, Kapuya aliongeza kusema, "Yeye sio wa kwanza kuoa mwanamke wa umri huo mdogo chamsingi ni kukubaliana tu, na siwezi tena kuoa mwanamke mwingine kwani mke huyu ni somo tosha, sababu mke wangu wa kwanza anaishi Dar nampenda sana ,huyu ni wa pili sasa natafuta nini tena kuoa? Hapa subirini tu mtoto kutoka kwa huyu mwanamke mnayesema ana umri mdogo,"alisema Kapuya.
Hata hivyo Kapuya amesema kwa mara ya kwanza amekutana na Mwajuma Kaliua, alipokuwa anaenda kufanyia vikao na Kaliua na Urambo sio mbali.