Kapombe mtu sana

KABLA hajajiunga na Simba, David Kameta ‘Duchu’ alifichua kwamba kwake Shomary Kapombe ni kila kitu na baada ya kutua amekiri kwamba jamaa ni mtu sana.

“Kwanza mashabiki wanapaswa kujua kuwa huu ni msimu wangu wa pili, baada ya kutoka Daraja la Kwanza nikacheza Lipuli kwa mara ya kwanza Ligi Kuu, kisha ikashuka, beki ambaye nilikuwa namkubali ni Kapombe,” alisema na aliongeza:

“Baada ya kusajiliwa Simba, nilimfuata na kumueleza jinsi ambavyo nilikuwa namfuatilia, kiukweli ni kaka ambaye anapenda mwingine afanikiwe, akaanza kunielekeza jinsi ya kujua thamani yangu, kujitambua, kujituma mazoezini na kuwa mvumilivu na aliniambia nina kitu kikubwa mguuni kwangu.

“Maisha yangu yamebadilika kwa sehemu, huwa nazingatia pia ushauri niliopewa na Kapombe ndio maana nakula kwa wakati, nalala kwa wakati, naamini uvumilivu wangu ndio utanifanya nionekana.

“Ngumu kuanza kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu Kapombe yupo kwenye kiwango cha juu, hivyo lazima niendelee kupambana ili nikija kupata nafasi nionyeshe makuu.”

Ukiachana na alichozungumza Duchu, beki wa zamani wa timu hiyo, Kasongo Athumani alisema anamuona mbali chipukizi huyo na kwamba kusajili Simba atajifunza vitu vingi kwa Kapombe.