Kapombe aipa pigo Simba, kuikosa Yanga

Muktasari:

  • Kapombe alijiunga na Simba mwaka 2017 akitokea Azam FC ambayo ilimnasa kutoka klabu ya AS Cannes ya Ufaransa

Mzimu wa nuksi umeanza kuikumba Simba, siku sita kabla ya mechi yake ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Yanga, baada ya beki wa kulia Shomary Kapombe kupata majeraha yatakayomfanya akose mechi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mtwara leo, kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema kuwa Kapombe atakosa mechi hiyo itakayochezwa Julai 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini kutokana na majeraha hayo aliyoyapata katika mechi ya robo fainali dhidi ya Azam wiki iliyopita
"Nadhani kila mmoja anafahamu majeruhi pekee tuliyenaye ni Kapombe ambaye atakuwa nje kwa wiki nne hivyo moja kwa moja hatocheza hadi msimu utakapomalizika," alisema Vandenbroeck
Kocha huyo alisema kuwa wachezaji wengine waliobakia wako fiti na wote wapo kwenye maandalizi ya mchezo huo wa Jumapili.
Kapombe alipata majeraha ya goti baada ya kufanyiwa faulo na Frank Domayo katika mchezo huo wa robo fainali uliochezwa Jumatano, Julai Mosi ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kuumia kwa Kapombe kunaamanisha kuwa Simba italazimika kuwatumia ama Haruna Shamte au Erasto Nyoni kucheza katika nafasi hiyo kwani ndio wamekuwa wakitumika pindi beki huyo anapokosekana.
Mkosi wa majeruhi kuelekea mechi hiyo ni kama umegeukia upande wa Simba sasa kwani wiki mbili zilizopita, kiungo wa Yanga, Mapinduzi Balama alivunjika mguu akiwa mazoezini, majeraha ambayo yatamfanya akose mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.
Vandebroeck alifichua kuwa baada ya mchezo wao dhidi ya Namungo kesho Jumatano, timu hiyo itabakia Kusini mwa Tanzania ambako itaweka kambi kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Yanga.
"Tuko katikati ya mechi mbili muhimu za vikombe. Tunatakiw kuendelea kucheza na kuonyesha taswira nzuri. Tunachokifanya sio kwa ajili ya matokeo bali kwa asilimia 100 ni kwa ajili ya mechi ya Jumapili.
Kwa hiyo maandalizi ya mchezo wa Namungo ni kwa ajili ya mechi ya Jumapili.
Tutaendelea kubakia hapa Mtwara kufanya mazoezi na tutaondoka siku ya mechi mapema asubuhi na baada ya mchezo wa Namungo tutarejea hapa Mtwara kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi dhidi ya Yanga," alisema Vandenbroeck.
Katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha Simba na Namungo kwenye Ligi Kuu msimu huu, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.