Kapombe Soka lake limempa mijengo ya maana

ANA sifa moja kubwa. Ni kutopenda kuzungumza sana mbele za watu lakini kazi yake huonekana dimbani. Ni kiraka Shomari Kapombe ambaye wakati mwingine unaweza kuhisi ana majivuno ila ndivyo alivyoumbwa.

Kapombe ukitaka kumfaidi basi ni uwanjani pekee anapokuwa kwenye majukumu yake, lakini kwa nje ya uwanja ni kwa wale ambao wana ukaribu naye ndiyo wanaoweza kuifaidi sauti yake kwa kupiga stori na kucheka naye.

Si kwamba hana majibu, ila ndivyo alivyo kwani hata ndugu zake wanaweka wazi Kapombe si mtu wa kuzungumza sana, anazungumza pale inapobidi, tofauti na wachezaji wengine wengi.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa mjini Morogoro kwa kazi maalumu ya kutembelea ndugu wa wachezaji mbalimbali wanaocheza soka ndani na nje ya nchi, lilizungumza na ndugu zake Kapombe akiwamo kaka yake Dizo pamoja na dada yake Halima Salum Kapombe.

Kapombe ni miongoni mwa wachezaji waliopita kwenye Kituo cha Moro Kids kilichopo Morogoro ambako ndiko nyumbani kwao wakiishi sehemu moja iitwayo Mafisa,

Simba ilimsajili Kapombe akitokea Polisi Moro na ilimchukua kwenye kituo hicho cha kulea na kukuza vipaji vya soka kwa vijana. Usajili wa Kapombe kwenda Simba ulifanywa msimu wa 2011 ambapo alidumu kikosini hapo hadi mwaka 2013.

Baadaye Kapombe alitimkia Cannes ya Ufaransa ambako alikaa kwa msimu mmoja pekee wa 2013/14 na kuamua kurudi nyumbani kutokana na sababu mbalimbali.

Akiwa nyumbani, Kapombe hakujiunga na Simba ambayo ilishindwa kumsaidia kutatua matatizo yake ya kisoka akiwa Ufaransa, hivyo akaamua kujiunga na Azam FC msimu wa 2014/2017.

Katika mahojiano baina ya Mwanaspoti na ndugu zake Kapombe ambao wamekuwa karibu naye kipindi cha nyuma kabla ya kuwa staa walieleza mambo kadhaa ambayo ndugu yao ameyapitia hadi kufikia hapo alipo. Kikubwa ni kumpongeza kwa juhudi zake ambazo zimempa mafanikio makubwa.

AZAM FC ILIILIPA CANNES

Baada ya kukwama kurudi Ufaransa, Kapombe alianza kutengenezewa zengwe na timu yake hiyo ya Cannes ambayo ilimsajili kwa mkataba wa miaka minne.

Kapombe wakati anavutana na Cannes alianza kufanya mazoezi na Azam FC kitendo hicho kilionekana kuwakwaza Cannes ambao baadaye walianza kumletea figusi za kutaka kumfungia endapo angesaini kwenye timu hiyo.

Wakati huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Jamal Malinzi, inadaiwa lilipokea barua kutoka Cannes ya kulalamikia mchezaji huyo kujiunga na Azam na Malinzi aliingilia kati kutatua Kapombe asifungiwe kwani pia ni tegemeo kwenye Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

“Hata Malinzi alisaidia vinginevyo wangemfungia miaka miwili, wao walitaka kama Kapombe anarudi Simba, basi klabu hiyo ilipe Euro 33,000 lakini kwenda Azam ilitaka ilipwe Euro 70,000.

“Kiukweli, Azam ilikuwa na nia na Kapombe ililipa kiasi hicho ndipo walipoacha kusumbua na kumwacha acheze Azam na kipindi hichohicho, alipewa gari aina ya Mark X ikumbukwe hapo alikuwa bado hajasaini mkataba,” anasema Dizo.

MIJENGO YAKE SASA

Kama hujui, Kapombe ni bonge la mchezaji mwenye akili ya kuona mbali aisee. Amewekeza kwenye ardhi ambapo jijini Dar es Salaam ana mijengo mitatu, ghorofa moja na nyumba za kawaida mbili, kwao Morogoro ana nyumba mbili sehemu moja inaitwa Kihonda na huko hadi mtaa ambao amejenga nyumba zake wameupa jina la Mtaa wa Kapombe.

“Kwa kweli mdogo wangu hata akistaafu ana sehemu ya kujishika, hajajisahau kama baadhi ya wachezaji walivyo, amewekeza kwenye ardhi kwa maana ya kwamba ana nyumba za kuishi Dar es Salaam na Morogoro, si haba. Huo ndio ujanja anacheza mpira kwa malengo maana soka ndiyo ajira yake pekee asipowekeza italeta shida baadaye,” anafafanua Dizo

PESA YA MAANA AZAM

Azam ndiyo timu inayoongoza kwa uwekezaji mkubwa katika soka, awali ndiyo timu ambayo pia ilikuwa inasemekana inalipa vizuri wachezaji kuanzia usajili hadi mishahara.

Miongoni mwa nyota walionufaika na pesa ya Azam ni Kapombe ambaye kwasasa anaichezea Simba.

Inaelezwa, Kapombe ndiye anayeongoza kwa kusajiliwa na pesa nyingi Azam kwa upande wa wachezaji wazawa ambapo usajili wake ulikuwa ni Sh150 milioni pamoja na gari, huku akipewa huduma mbalimbali muhimu.

“Ni kweli kama ulivyosikia kuwa alilipwa pesa nzuri, Azam wamemsaidia Kapombe sana hata yeye huwa anasema, sidhani na sitarajii kama Kapombe anaweza kuidharau Azam, hayupo hivyo anatambua na anathamini kile ambacho Azam imefanya juu yake, ukimya wa Kapombe huwa unamaanisha mambo mengi moyoni mwake, hata alipoenda Simba si kwamba aliwadharau Azam,” anasema.

ABADILISHA MAISHA YA NYUMBANI

Imeelezwa aliporudi kutoka Ufaransa alikuta nyumbani kwao wamekatiwa umeme na Tanesco kwani walikuwa wakidaiwa, kitendo hicho kilimsononesha na kuamua kwenda benki na ndugu yake ili wakalipe deni.

“Kwa kweli Kapombe ametufanyia mengi mazuri, tunaendelea kujivunia. Hata aliporudi kutoka Ufaransa alilipa deni la Sh 2 milioni tulilokuwa tunadaiwa na Tanesco hadi walitukatia umeme, tulikaa miaka miwili bila umeme.

“Alifanya mambo ambayo yanampa baraka kwenye kazi yake ikiwemo kujengea makaburi ya wazazi wake na ndugu zetu wengine, hiyo ni baraka kubwa sana kwake, kiukweli maisha yetu yalibadilika kupitia Kapombe kabla hawajazuia pesa yake.

“Siku moja tumeenda kwenye ATM ndipo tulikutana na janga hilo, pesa hazikutoka na tulipouliza tulielezwa kuwa zimezuiwa kwasababu haijaeleweka kama mwenye hizo pesa bado yupo Ufaransa ama wapi. Hapo ndipo tabu zilipoanzia, hatukuwa na namna nyingine maana ndugu yetu alikuwa nyumbani,” anakumbuka.

ALILALA UWANJA WA NDEGE

Imeelezwa kuwa baada ya visa kumsumbua ilimbidi atafute ya muda lakini alipofika Uwanja wa Ndege wa Kenya alizuiwa. Kuzuiwa kwake kulimfanya alale uwanjani hapo na kulazimika kurudishwa Tanzania na safari yake ya Ufaransa ikawa imeishia hapo.

“Ndiyo maana nasema mdogo wetu ni mpambanaji na hakati tamaa, amekuwa akisimamia misingi yake na anaamini kile anachokifanya, alifanya jitihada zote ili arudi Ufaransa matokea yake aliishia kulala Uwanja wa Ndege Kenya.

“Sio kwamba aliumia peke yake, hata sisi ndugu tuliumia kwani tuliona mambo ndiyo yameharibika, pesa nayo ilizuiwa basi ilikuwa balaa tupu ila Denis Kadito (ambaye alikuwa wakala wake) huenda aliujua mchongo mzima wa ndugu yetu,” anasema Dizo

KASEJA, OKWI, BOBAN, NGASSA WAHUSIKA

Watu wengi huenda wamechangia mafanikio ya Kapombe ukiachana na juhudi zake mwenyewe, kutokata tamaa na kuipenda kazi yake, lakini baadhi ya nyota wenzake wamekuwa na mchango hata wa kimawazo hadi hapo alipofikia Kapombe.

Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Haruna Moshi ‘Boban’, Mrisho Ngassa wametajwa kuwa ni miongoni mwa wale waliokuwa wanampa moyo Kapombe kwenye maisha yake hayo ya mpira ikiwemo ushauri.

“Nakumbuka Kaseja aliwahi kumwambia kuwa ajitahidi awekeze sana kwenye ardhi kwani utajiri ni nyumba na sio magari, Okwi na Boban walimpigania sana kwa kocha ikiwa ni mara yake ya kwanza kuichezea Simba na alipotua tu walikuwa wanajiandaa na mechi dhidi ya Yanga.

“Kweli kocha alimpa dakika 14 na alionyesha kiwango kizuri, Okwi aliwahi kumuona wakati wa michuano yao ya U-23 na yeye alikuwa kwenye kikosi chao cha Uganda, hivyo alifahamu kiwango chake, Boban yeye alipomuona tu alijua dogo ni mchezaji mzuri, hivyo walikuwa wanampa moyo sana hasa ukiangalia umri ulikuwa mdogo.

“Ngassa pia ana mchango wake wa Kapombe kwani alikuwa anampitia na gari yake kwenda mazoezini, Ngassa tayari alikuwa maarufu na mwenye uwezo wake. Wapo wengi ambao hatuwezi kuwashukuru mmoja mmoja,” anafafanua Dizo.

KIDOGO ATUE YANGA

Mambo ya usajili achana nayo kabisa, unaweza kukaa ukimsubiri mchezaji umsainishe lakini kumbe wenzako wamemdaka juu kwa juu na wamemalizana naye, ndivyo ilivyotokea kwa Kapombe wakati anatoka Polisi Moro akiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye alikuwa ana mpango wa kumpeleka Simba lakini alianza kwanza kucheza na akili ya Yusuf Manji wakati huo ni Mwenyekiti wa Yanga.

“Unajua Kapombe alivyoitwa kwenye Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23 wakati huo Julio alikuwapo huko, alimkutanisha na Manji ili asajiliwe Yanga, walifanya mazungumzo na kukubaliana kumalizana kesho yake saa 4 asubuhi, kilichotokea ile wanatoka tu ofisini kwa Manji pale Quality Plaza wakamkuta Kaburu (Geofrey Nyange) amepaki gari lake nje linawasubiri.

“Nahisi huu mchongo, Julio alikuwa anaujua na kuwaambia Simba kinachoendelea, Manji alikuwa tayari kumpa Kapombe Sh 15 milioni, hivyo Kaburu alivyomchukua pale walikwenda kumalizana naye siku hiyohiyo na kwa pesa hiyo aliyoahidiwa na Manji, mchezo uliishia hapo,” anasema Dizo.

SIMU ILIPIGWA AKIWA KWENYE NDONDO

“Nakumbuka Julio alipiga simu ya kumhitaji Kapombe kujiunga na timu hiyo tukiwa kwenye mechi ya ndondo, changamoto ikawa kwenye nauli, hapo hakulipwa mishahara ya miezi mitatu na Polisi Moro, ambapo kwa mwezi alilipwa Sh 48,000.

“Ili ndugu yetu aende Dar kujiunga na timu hiyo ambayo kiukweli ilikuwa ni bahati kubwa kwake na kwetu kama familia, ilibidi familia ichangishane ipatikane nauli ya kwenda huko, kweli kesho yake kama alivyohitajika alianza safari na maisha yake ya mafanikio yaianzia hapo,” anaeleza

ALIZIMIA UWANJANI

Wakati Kapombe anajiandaa kwenda Ufaransa, mipango ikiwa imakamilika kabisa alikwenda nyumbani kwao Morogoro kuwaaga lakini alipofika huko alikuta timu ya ndugu yake Dizo inacheza fainali za Mpira Pesa Uwanja wa Shule ya Msingi Mafisa, si akavaa jezi na kuingia kucheza kilichotokea sasa.

“Unajuwa Kapombe anapenda sana mpira, yaani anapenda mno. Alikuja kutuaga wakati anataka kwenda Ufaransa, sasa timu yangu ya mtaani ilikuwa inacheza fainali, hivyo nilimlazimisha kweli kucheza japokuwa ingawa yeye hakuwa tayari kuucheza mchezo huo kwa kuhofia kuumia.

“Nilimbembeleza sana na kwa vile mimi ni ndugu yake alikubali, alicheza na hapo tulikuwa tumefungwa bao moja, alivyoingia tu akafunga bao la kusawazisha baadaye alichezewa rafu akaangukia kichwa na kuzimia kabisa.

“Lakini baada ya kuzinduka nilidhani asingeweza kuendelea na mchezo, aliingia uwanja kuendelea na mechi tulipata penalti ambayo alipiga yeye hivyo tulichukua ubingwa kwa ushindi wa bao 2-1.

Kila bao lililokuwa linafungwa lililipwa Sh 20,000 hivyo alipata 40,000 ila hakuondoka nazo yeye alimpa rafiki yake,” anasema.

KAPOMBE NI BABA

Mtoto wa kwanza wa Kapombe anaitwa Shadya na mwingine Ester. Dada yake Kapombe aitwaye Halima Salum Kapombe anaelezea hisia zake juu ya mdogo wake na shangazi zake hao.

“Huwa namuombea sana mdogo wangu afanikiwe zaidi ya hapa, kwani kupitia yeye maisha yetu yalibadilika, ni kijana mpole hata akija hapa huwezi kujua kama yupo ndani, anapenda zaidi kucheza michezo ya kwenye televisheni (game).

“Kwa kweli nawapenda sana watoto wa Kapombe ambao ni shangazi zangu, hata akinipa niishi nao nipo tayari kuwalea maana ni damu yangu.

“Upendo anaotuonyesha sisi kwanini tushindwe kuwapenda watoto wake ama familia yake,” anasema

Hata hivyo, ndugu hao wanaumia sana pale Kapombe anapopata mitihani ya kuumia mara kwa mara. Na wanamuombea Mungu ili apone na kurudi uwanjani.