Kapombe, Manula wakamua mamilioni Simba

Sunday May 19 2019

 

By WAANDISHI WETU

MASHABIKI wa Simba bila shaka wanafurahia kusikia taarifa za nahodha na mshambuliaji wao kipenzi, John Bocco kusaini mkataba mpya wa kutumikia timu hiyo, lakini kabla furaha hiyo haijaipoa uongozi umewafanyia sapraizi nyingine kwa kuviongezea mkataba vifaa vingine viwili. Vifaa hivyo kama ilivyokuwa kwa Bocco, vilikuwa kwenye hatari ya kutoweka Msimbazi.

Nyota hao wawili ambao wameungana na Bocco kusaini mkataba mpya wa kuitumikia Simba ni kipa tegemeo wa timu hiyo Aishi Manula na beki kiraka Shomary Kapombe, ambao kila mmoja ameongeza mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Simba.

Kapombe na Manula kama ilivyo kwa Bocco ni miongoni mwa wachezaji takribani nane ambao, mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu na Simba ilikuwa ikihaha kuwabakiza kutokana na mchango mkubwa ambao, wamekuwa wakiutoa kikosini.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezinasa kutoka kwa chanzo kilicho karibu na wachezaji hao, zimethibitisha kuwa Manula na Kapombe walisaini mikataba hiyo mipya juzi Ijumaa wakiwa sambamba na Bocco, ambaye taarifa za kusaini kwake ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na Mwanaspoti.

“Kama ilivyo kwa Bocco, Manula na Kapombe nao wamesaini jana (juzi) Ijumaa hivyo wataendelea kuitumikia Simba kwa mara nyingine na rasmi tetesi za wao kujiunga na timu nyingine kama wachezaji huru zimekufa,” kilithibitisha chanzo hicho.

Manula na Kapombe wamesaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja ingawa kiasi cha fedha walichovuna baada ya kumalizana na Simba hakijawekwa wazi. Hata hivyo, inaaminika kuwa dau la Kapombe na Manula linaweza kulingana na la Bocco. Taarifa za awali zinaeleza kwamba, straika huyo tishio amesaini dau kati ya Sh 60-80 milioni.

Advertisement

Kapombe licha ya kukumbwa na majeraha yaliyomweka nje muda mrefu msimu huu, ni miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba msimu uliopita kilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupitisha misimu mitano mfululizo bila kufanya hivyo.

Katika msimu uliopita, Kapombe alikuwa akichezeshwa kwenye nafasi tofauti uwanjani ambazo alimudu kuzitumikia vyema akianza kama beki wa kulia na baadaye akipangwa kama kiungo namba sita na pia kocha Pierre Lechantre wakati mwingine alimtumia kama winga wa kulia, kiungo namba nane na pia namba 10.

Hata hivyo, mwanzoni mwa msimu alipata majeraha wakati wa maandalizi ya Kambi ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa ikijiandaa na mechi ya ugenini ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Lesotho, yaliyomweka nje hadi sasa

Kwa upande wa Manula, tangu alipojiunga na Simba akitokea Azam FC, amekuwa kipa chaguo la kwanza akiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13 tu kwenye ligi na kufanikiwa kuchukua tuzo ya Kipa Bora wa msimu uliopita na kuna dalili zote za kubeba tena tuzo hiyo msimu huu.

Wawili hao kama ilivyo kwa Bocco walikuwa wakihusishwa na klabu yao ya zamani ya Azam FC, ambayo ilikuwa kwenye mpango kabambe wa kuwarudisha baada ya kushindwa kuwaongezea mikataba pindi ile ya awali ilipomalizika mwishoni mwa msimu wa 2016/2017.

Ni wazi sasa presha imeshuka kwa upande wa Simba ambayo sasa imebakiza jukumu la kuhakikisha nyota wake wengine tegemeo, Jonas Mkude, James Kotei, Erasto Nyoni, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima wanasaini mikataba mipya ya kuitumikia timu hiyo.

AUSSEMS AACHA MSALA

Achana na ishu ya Kapombe na Manula kusaini mikataba mipya, Simba leo inashuka uwanjani kuikabili Ndanda ikiwa kwenye harakati za kuhakikisha inatetea ubingwa wake. Baada ya Ndanda leo Jumapili, Simba itaendelea na kampeni zake kwa kuifuata Singida United, Biashara United na Mtibwa Sugar na katika michezo hiyo iliyobaki inatafuta pointi nne tu kutetea ubingwa wake.

Simba inaingia uwanjani kuikaribisha Ndanda ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 3-0, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Ndanda waliifunga Africa Lyon bao 1-0.

Simba mpaka sasa imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 14, katika michezo 34, imefunga mabao 72, ambayo kati ya hayo washambuliaji watatu Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco imefunga jumla ya mabao 50. Kagere anaongoza kwa kufunga akiwa na mabao 20 kwenye mechi za Ligi Kuu Bara wakati Okwi na Bocco kila mmoja ana mabao 15.

Wakati Simba akionekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji msimu huu kocha wa kikosi hicho Patrick Aussems, alisema hashangazwi na kasi ya washambuliaji wake kwani kabla ya msimu huu kuanza aliamini wataifanya vyema kazi hiyo.

“Ukiangalia kwa makini aina yetu ya uchezaji tunapenda kumiliki mpira na kushambulia na hapo washambuliaji wanashindwa vipi kufunga mabao ya kutosha na kama wasingeweza kufanya hivyo ningeshangaa sana.

“Binafsi sishangazwi na mabao 50 yaliyofungwa na Kagere, Okwi na Bocco hiyo ndio kazi yao ya kwanza lakini naamini timu inacheza vizuri, walitakiwa kufunga zaidi ya hayo.

“Tumebakiwa na michezo minne iliyobaki nataka waongeze kasi ya kufunga na idadi kubwa ya mabao na hilo litawezekana kwa kutumia nafasi ambazo timu inatengeneza,” alisema na kuongeza.

“Kila mwalimu lazima awe na mipango yake, hivyo ndio ilivyo kwangu kila mchezaji ana jukumu kutokana na sehemu ambayo anacheza na tulikubaliana hili kabla ya ligi kuanza, tulifanya hivyo kufikia malengo tuliyojiwekea.”

Wechazaji wengine wa Simba wenye mabao mengi ni kiungo Mzambia Cletous Chama mwenye mabao sita akifuatiwa na Adam Salamba aliyefunga mabao manne.

Kwa upande wa Kocha wa Ndanda FC, Khalid Adam alisema ugumu wa mechi hiyo utatokana na kukutana na timu mbili zenye malengo tofauti kuelekea kumaliza ligi msimu huu.

Alifafanua kauli yake, Simba wapo kwenye harakati ngumu za kutetea ubingwa, jambo ambalo analiamini wataingia uwanjani kwa ushindani wa hali ya juu, lakini kwa upande wao ni kujiweka kwenye mazingira mazuri.

“Pointi za mchezo wa kesho (leo), zitakuwa za kinyang’anyiro na mwenye nguvu ndiye atakayefanikiwa kutoka kifua mbele dakika 90 za mchezo, upande wetu tutaingia uwanjani kwa kuwaheshimu Simba ila tukijua tunachokitaka kwao.

“Kikosi cha wapinzani wetu kipo vizuri ukitaka kujua hilo ni jinsi ambavyo safu yao ya mbele inavyozalisha mabao, umakini wetu ndio utatupa pointi tatu, kikosi kipo tayari kwa ajili ya kazi.

MO DEWJI ATINGA KAMBINI

Katika hatua nyingine Mwenyekiti ya Bodi wa Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ juzi Ijumaa alikutana na wachezaji wa timu hiyo katika hoteli ya Sea Scape ambako ndiko imeweka kambi yao.

Mo Dewji alikutana na wachezaji hao kwa ajili ya chakula cha usiku baada ya kupata futari na viongozi wa Simba katika hoteli ya Serena.

Mo Dewji alizungumza na wachezaji kuhusu kupambana na kujitolea katika mechi zilizobaki za ligi ili kufanikisha kutwaa ubingwa msimu, kwani mara ya mwisho kukutana na wachezaji ilikuwa Februari 12, siku ambayo walicheza na Al Ahly.

IMEANDIKWA NA CHARLES ABEL, MWANAHIBA RICHARD

THOBIAS SEBASTIAN NA OLIPA ASSA

Advertisement