Kanuni mpya EPL utata mtupu

Muktasari:

  • Ligi Kuu England itarudi rasmi Juni 17 baada ya kusimamishwa tangu Machi mwaka huu ikiwa ni hatua za serikali ya Uingereza kukabiliana na virusi vya Corona.

London, England. Kanuni mpya ambazo zitatumika katika mechi zilizobaki za Ligi Kuu ya England msimu huu zinadaiwa kuleta mgawanyiko baina ya timu 20 zinazoshiriki Ligi hiyo.
Kati ya kanuni hizo, tatu ndizo zinazoobeka kuleta mgogoro zaidi ambazo ni ile ya kuongeza idadi ya wachezaji wanaofanyiwa mabadiliko, klabu kuruhusiwa kufanya usajili wa muda na nyingine ni ile ya uwingi wa mipira uwanjani.
Wakati baadhi ya klabu zikiunga mkono kanuni hizo, inadaiwa kuwa kuna klabu ambazo zimepanga kugomea kanuni hizo mpya zilizotungwa hivi karibuni ikiwa ni matokeo ya tatizo la virusi vya Corona vilivyopelekea ligi kusimama.
Kundi kubwa la klabu linadaiwa kusapoti uamuzi wa kuongezeka idadi ya wachezaji wanaofanyiwa mabadiliko kutoka watatu hadi watano kutokana na hofu ya majeraha baada ya mapumziko ya muda mrefu huku Chelsea wakipendekeza idadi ya wachezaji kwenye benchi iongezeke kutoka saba hadi tisa.
Kanuni nyingine ni ile ya timu kuruhusiwa kusajili wachezaji wa ziada ambao hawakuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji 25 ambao majina yao yalisajiliwa kutumika kwa msimu huu.
Licha ya wengi kufurahishwa na kanuni hizo, inatajwa kuwa kuna kundi la klabu zimepanga kupinga na klabu hizo ni zile ambazo hazina vikosi vipana hasa vya vijana.
Pamoja na hilo, klabu kadhaa pia zinadaiwa kujipanga kuipinga kanuni ya uwepo wa idadi kubwa ya mipira viwanjani kwa sababu itawafanya wachezaji kukosa angalau sekunde kadhaa za kupumzika pindi mechi inapokuwa inaendelea.
Baadhi ya makocha wanaamini kwamba pindi mpira unapotoka nje inasaidia mchezaji kupata sekunde kadhaa za mapumziko jambo ambalo haliwezi kutokea ikiwa kutakuwepo na mipira mingi kwani itakuwa inarudishwa kwa haraka kiwanjani.
Hata hivyo mbivu na mbichi zitakuja kujulikana keshokutwa Alhamisi ambapo klabu hizo 20 zitapiga kura ya kupitisha au kugomea kanuni hizo.
Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa wa upitishaji kanuni, ili kanuni ipitishwe inahitajika angalau kura za klabu 14 kati ya 20.