Kanda awaacha Yanga kwenye mataa
Muktasari:
YANGA kupitia kwa wadhamini wao, GSM walikuwa kwenye mikakati ya chinichini ya kuangalia uwezekano wa kuwafanyia sapraizi Simba.
YANGA kupitia kwa wadhamini wao, GSM walikuwa kwenye mikakati ya chinichini ya kuangalia uwezekano wa kuwafanyia sapraizi Simba.
Walitaka kumsajili, Deo Kanda ambae alikuwa Simba kwa mkopo kutokea TP Mazembe ya DR Congo.
Yanga walishazungumza mpaka na wakala wake ambaye aliwaelekeza kwa Mazembe, huku ikidaiwa walikuwa wakimtumia Papy Tshishimbi kumshawishi.
Lakini habari za ndani ambazo Mwanaspoti imezipata ni mchongo huo umekufa baada ya Simba kumwekea mkataba wa miaka miwili mezani.
PICHA LILIVYOKUWA
Kanda alikuwa na mkataba wa miezi sita na Simba, ambao unamalizika mwisho wa msimu huu, lakini uongozi wa timu hiyo kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingiza fasta baada ya kufahamu mchongo huo ulimwita mchezaji mezani.
Kanda akiwa na mmoja wa mawakala wake alikutana na Simba wiki iliyopita na mwenyewe alikiri kunyemelewa na Yanga kutokana na baadhi ya viongozi wa timu hiyo kumfuatilia na kutaka kumvuta kwao kwa ajili ya msimu ujao.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni Kanda, aliwaacha Yanga kwenye mataa na wiki iliyopita Ijumaa Simba walimpa mkataba ambao muda wowote atausaini na kuwarejeshea kwani wameshakubaliana kila kitu.
Zoezi hilo lilifanyika kimya kimya kwenye ofisi za klabu hiyo Posta, katika gorofa la Diamond, Jijini Dar es Salaam.
Senzo alipotafutwa alisisitiza kila mchezaji ambaye yupo katika mipango yao kwa ajili ya msimu ujao hataondoka na wale wanaomaliza mikataba wataongezewa.
“Tunafahamu tuna jukumu kubwa la kuwabakisha wachezaji wetu ambao wanamaliza mikataba lakini hilo hatuna wasi wasi nalo kwani kila kitu kitakwenda sawa kama ambavyo benchi letu la ufundi ambavyo litakuwa linahitaji,” anasema Senzo.
Ingawa mchezaji huyo hajataka kuzungumza lolote kuhusu mkataba mpya, Kocha wa Yanga, Luc Eymael alikiri ni ngumu kumpata mchezaji kutoka Simba kama wakiwa na mahitaji nae katika kipindi hiki, ndio maana yeye hajapendekeza mchezaji yeyote kutoka kwao licha ya kuhusishwa pia na Clatous Chama.
“Nadhani zilikuwa kama drama kwa ambavyo Simba inataka kujijenga na kuimarika ilikuwa ngumu kutuuzia mchezaji kama Kanda kwani hata nasi tupo katika harakati za kufanya usajili wa maana ambao hautakuwa na makosa ndani yake kama msimu uliopita,” anasema Eymael.
“Tupo sokoni na kweli tunatafuta winga mwenye uwezo ambaye tuna imani tutapa aliyokuwa bora zaidi ya Kanda ambaye atakuja kuleta tija ndani ya timu kwa maana ya kufanya vitu ambavyo timu itakuwa inahitaji kutoka kwake,” alisema Eymael ambaye rada yake ya kusaka wachezaji ipo DR Congo na Rwanda.
KUTUA SIMBA
Alijiunga rasmi na Simba, Julai, 2019 kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja akitokea TP Mazembe ya DR Congo ambayo ameitumikia tangu mwaka 2009 akitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili, Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili lakini pia wakitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya DR Congo zaidi ya mara sita.
Kwa muda wa miezi sita Kanda amekuwa mchezaji wa kutegemewa katika kikosi cha Simba, akihusika katika kutengeneza mabao na kufunga akiwemo katika mechi ya mzunguko wa kwanza dhidi ya watani zao Yanga.
MABAO SABA
Amehusika katika mabao mengi waliyofunga wachezaji wenzake.
Kama hilo halitoshi Kanda amefunga mabao saba katika ligi mpaka sasa huku akionekana kucheza mechi chache lakini kwa kiwango cha kuvutia.
Kupiga chenga, kukimbia na kusimama haraka katika nafasi sahihi, kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao, ni mambo ambayo yatainufaisha zaidi Simba misimu miwili ijayo.
Ni wazi katika wachezaji waliokuwa kwenye ligi, Kanda ameonyesha kiwango bora katika kumiliki mpira, kutengeneza nafasi za kufunga, kupiga vyenga na hata muda mwingine kufanya mwenyewe.
Kanda uzoefu wake kwa soka la Afrika na Tanzania kiujumla, vitakuwa na faida kwa Simba msimu ujao kwani ni mchezaji ambaye hatohitaji kupewa muda kuzoea na kuhimili mazingira na mfumo na staili ya kiuchezaji katika mashindano makubwa.
Uzoefu huo ameupata kwa kucheza ligi za nchi tofauti kama vile DR Congo, Angola, Ugiriki, Morocco na Tanzania, pia amecheza katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
Kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi ya winga, Simba inaweza kumpanga katika mfumo wa (4-4-2) akicheza kulia au kushoto, anaweza kutumika katika mfumo wa (4-2-3-1), akicheza kama kiungo wa ushambuliaji wa pembeni na kushindana na mabeki wenye uwezo kutoka katika klabu nyingine kubwa Afrika au hata hapa ndani.
MSIKIE MWENYEWE
Wakati mkataba wake ukiwa unaelekea ukingoni kabla ya Ligi Kuu Bara kusimana Kanda aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa malengo yake makubwa ni kuendelea kusalia katika klabu hiyo na kucheza kwa muda mrefu zaidi ya hiyo miezi sita aliyosaini hapo awali.
“Nipo na ofa nyingi kutoka katika maeneo mbalimbali lakini natamani kubaki na kuendelea kucheza soka la hapa Tanzania hasa katika klabu yangu ya Simba lakini kama linaweza kutokea lolote nitaeleza pia wakati ukifika,” anasema.
“Najua mashabiki wa Simba wananipenda na hii ni namna wanavyoishi na mimi. Nafurahi kwa kweli, ndio maana napambana ili niendelee kucheza hapa kwa muda mrefu,” anasema Kanda.