Kambi ya Moro Bigirimana, Kalengo wafunika

Muktasari:

  • Utekelezaji wa ratiba hiyo ni kwamba Mwandila amekuwa mkali kuhakikisha kila mchezaji anafanya mazoezi hayo kwa uwezo mkubwa huku wachezaji nao wakionyesha juhudi kubwa.

YANGA ipo mjini Morogoro kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya, lakini ratiba ya mazoezi yao huko ni jasho zito baada ya nyota wa timu hiyo kukimbizwa vibaya.

Yanga imejichimbia kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia cha Bigwa nje kidogo ya mji ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano sambamba na kutambulisha nyota na jezi mpya, kwenye tamasha maalumu la Siku ya Wananchi litakalofanyika Agosti 3 jijini Dar es Salaam.

Kikosi hicho cha Yanga kinaingia siku ya nne leo Alhamisi katika kambi hiyo iliyopo kule milimani Bigwa kikiwa chini ya Kocha Msaidizi Noel Mwandila na unaambiwa moto umekuwa mkali katika mazoezi hayo kwa wachezaji kujazwa pumzi ili mengine yaendelee.

Ratiba kamili ilianza Jumatatu jioni na mpaka jana asubuhi ratiba kubwa iliyochukua nafasi ni mazoezi ya pumzi na stamina, ambapo kiasi kikubwa zilikuwa ni mbio za kutosha, huku baadhi ya nyota wa kigeni wakifunika mwanzo mwisho.

Utekelezaji wa ratiba hiyo ni kwamba Mwandila amekuwa mkali kuhakikisha kila mchezaji anafanya mazoezi hayo kwa uwezo mkubwa huku wachezaji nao wakionyesha juhudi kubwa.

SIKU MBILI BILA KUGUSA MPIRA

Juzi jioni kidogo dozi hiyo ya mbio ilionekana kupunguzwa baada ya wachezaji kugusa mpira nyakati za jioni, lakini jana asubuhi ratiba ya mbio kali ikarejea tena kwa kasi, kisha jioni wakagusa mpira kidogo.

Inaelezwa Mwandila na wenzake waliwapa wachezaji hao mazoezi ya kukimbia ambayo wakitumia kati ya dakika 45-60 kwa kutambua kuwa wengi wametoka mapumzikoni baada ya kumalizika kwa ligi, hivyo kukimbia kungewapa kasi kabla ya kuanza kufundishana ufundi na mbinu ikiwa ni mwanzo wa kuanza kazi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara iliyotangazwa kuanza Agosti 23.

KALENGO, BIGIRIMANA NOMA

Katika mazoezi hayo ni kwamba nyota wapya karibu wote wako kambini kasoro straika Sadney Urikhob na kipa Farouk Shikalo, lakini mastraika Maybin Kalengo na Issa Bigirimana walionekana kuhimili kwa kishindo mazoezi hayo wakiwa na kasi nzuri.

Kinachowasaidia zaidi mastraika hao pia ni kuwa na kasi hasa nafasi za viungo wa pembeni wanazomudu kucheza ambapo hawakuwa na shida katika mazoezi hayo, huku beki Lamine Moro na Patrick Sibomana nao wakionekana kuwa sawa.

Wachezaji hao ni kati ya nyota 10 wapya waliosajiliwa na Yanga wakiwamo Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Ally Mtoni ‘Sonso’, Ali Ali, Juma Balinya na Mustapha Seleman.

Mmoja wa wajumbe waliopo kwenye kambi hiyo ameeleza kuanzia jioni ya jana Jumatano wachezaji walirejea uwanjani kugusa mpira na kuanza kufundishwa mbinu, lakini kazi inaelezwa itakolea zaidi atakapotua Kocha Mkuu Mwinyi Zahera aliyekwenda Ufaransa kwa muda akitokea kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

“Vijana wako vizuri na mazoezi yanaendelea, lakini kwa sasa tumeimarisha sana ulinzi kwenye kambi yetu. Mashabiki wasiwe na hofu kabisa, msimu ujao mambo yatakuwa moto kwelikweli,” alisema mjumbe huyo.