Kambi popote : Wachezaji wa ndani walipogeuzwa makipa

Muktasari:

Hii hapa orodha ya wachezaji wa ndani waliowahi kuwekwa golini kudaka baada ya makipa wa timu husika kukabiliwa na matatizo mbalimbali, kitu kilichowahi kumhusu pia beki wa kulia Dani Alves alipodaka wakati huo akiwa na PSG kwenye mechi ya Kombe la Ufaransa dhidi ya Sochaux baada ya kipa Kevin Trapp kutolewa kwa kadi nyekundu. Lakini, kuna wachezaji wengine hawa hapa

LONDON,ENGLAND . INATOKEA mara chache sana, lakini ndio hivyo kuna nyakati timu inakuwa njiapanda na kuhitaji mchezaji wa ndani kwenda kukaa golini kama golikipa.

Lakini kumtazama mchezaji wa ndani akicheza mechi kama kipa ni kitu kinachovutia kwelikweli na kutia raha.

Usiku wa juzi Jumatano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester City ilihitaji huduma ya beki wake, Kyle Walker kuwajibika kama kipa baada ya mwenye nafasi hiyo, Claudio Bravo kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Josip Ilicic wa Atalanta akiwa mtu wa mwisho.

Beki huyo wa kulia, Walker alilazimika kutupia kwenye mavazi ya makipa na kukaa golini kwenye mchezo huo na hakika aliokoa hatari nyingi kuliko walivyofanya Ederson na Bravo katika mechi hiyo.

Hii hapa orodha ya wachezaji wa ndani waliowahi kuwekwa golini kudaka baada ya makipa wa timu husika kukabiliwa na matatizo mbalimbali, kitu kilichowahi kumhusu pia beki wa kulia Dani Alves alipodaka wakati huo akiwa na PSG kwenye mechi ya Kombe la Ufaransa dhidi ya Sochaux baada ya kipa Kevin Trapp kutolewa kwa kadi nyekundu. Lakini, kuna wachezaji wengine hawa hapa

11) Kyle Walker – Atalanta vs Man City, 2019

Wakati Kyle Walker alipoanzia benchi kwenye kikosi cha Manchester City kilichomenyana na Atalanta usiku wa juzi Jumatano, hakuwa na uhakika kabisa kama atacheza mechi hiyo akiingia kwenye nafasi ya kipa. Kipa namba moja wa Man City, Ederson alitolewa wakati wa mapumziko na kuingia Claudio Bravo, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu zikiwa zimebaki dakika 10. Kocha Pep Guardiola alitazama kwenye benchi lake na kumwinua beki wa kulia, Walker kwenda kuziba pengo la Bravo uwanjani, ndipo alipovaa glovu na kutolewa Riyad Mahrez ili Mwingereza huyo akawe kipa na Man City wakicheza 10. Shughuli ya kwanza ya Walker ilikuwa kuzuia friikiki na alisaidia timu yake isifungwe na kupata sare ya 1-1 ugenini huko Italia.

10) Harry Kane – Tottenham vs Asteras Tripoli, 2014

Harry Kane hakuwa huyu Kane anayefahamika kwa sasa kipindi hicho, Oktoba 2014. Alikuwa bado ni mchezaji wa kawaida sana kwenye kikosi cha kwanza cha Tottenham. Kwenye mechi moja ya Europa League, dhidi ya Asteras Tripoli, kipa Hugo Lloris alitolewa kwa kadi nyekundu dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho na hapo Spurs ilikuwa imemaliza sub zake, ikalazimika Kane kuwa kipa. Kane alishindwa kudaka shuti la Jeronimo Barrales, mpira ukiponyoka mikononi na kuwa bao. Kabla ya kuwa kipa, Kane alikuwa amefunga hat-trick kwenye mechi hiyo kuisaidia Spurs kushinda 5-1. Erik Lamela alifunga mawili.

9) John Terry – Chelsea vs Reading, 2006

Kumpoteza kipa mmoja kwa majeruhi kwenye mechi ni bahati mbaya, lakini kumpoeza kipa wa pili ndani ya mechi hiyo hiyo ni mkosi. Hilo lilitokea wakati Chelsea ilipokipiga na Reading, 2006 na Petr Cech alijigonga na Stephen Hunt akaumia akatolewa uwanjani, kisha akaingia Carlo Cudicini, ambaye pia aliumia baada ya kugongana na Ibrahima Sonko. Baada ya hapo, beki wa kati John Terry akalazimika kwenda kuwa kipa na kumalizia dakika zilizokuwa zimebaki kwenye mchezo huo.

8) Mia Hamm – Marekani vs Denmark, 1995

Si kitu cha kawaida kwa makocha wote wawili kutokubaliana na mwamuzi, lakini hilo lilitokea 1995 kwenye Kombe la Dunia la timu za Soka za Wanawake, wakati kipa wa Marekani, Briana Scurry alipotolewa kwa kadi nyekundu na jambo hilo ndilo lililowafanya Marekani kulazimika kumtumia mchezaji wa ndani kama kipa, Mia Hamm alipokwenda golini kumalizia dakika sita zilizokuwa zimebaki kumaliza mechi. Hamm, aliyesema kwamba alikuwa kwenye woga mkubwa wa kuwa kipa, aliokoa na kufanya timu yake isifungwe.

7) John O’Shea – Man United vs spurs, 2007

Kuna nyakati hizo, Tottenham Hotspur kama ilikuwa nzuri kiasi gani kwenye mechi yake dhidi ya Manchester United ilipigwa tu. Kuna mechi hiyo, Man United iliipiga Spurs bila hata ya kipa golini kwao. Hiyo ilikuwa mwaka 2007, wakati kipa Edwin van der Sar alipovunjika pua na hapo Man United ilikuwa mbele kwa mabao 4-0, ikimaliza sub zote ndipo John O’Shea alipolazimika kwenye golini kucheza nafasi ya kipa na hakika alikoa hatari moja matata dhidi ya Robbie Keane.

6) Jackie Blanchflower – Man United vs Aston Villa, 1957

Hii ilikuwa kali zaidi. Mechi ilionekana kama vile imeshakwisha wakati mchezaji wa ndani alipolazimika kwenda kukaa golini kucheza nafasi ya kipa. Hii ilikuwa kwenye fainali ya Kombe la FA 1957, wakati kipa wa Man United, Ray Wood alipoumizwa na winga wa Aston Villa, Peter McParland na kuvunjika taya katika dakika ya sita tu. Hakukuwa na sub, hivyo beki Jackie Blanchflower akalazimika kuwa kipa na ilikuwa shughuli ambapo McParland alifunga mara mbili, Villa ikishinda 2-1. Baadaye, Wood alirudi uwanjani kama mchezaji wa ndani na kwenda golini katika dakika saba za mwisho.

5) Alain Giresse – Bordeaux vs Nantes, 1982

Mechi ya mwisho kabisa ya msimu na ilikuwa ya aina yake kutokana na kile kilichotokea. Bordeaux ilipata pigo ambapo kipa wake namba moja, Dragan Pantelic alikuwa na adhabu, hivyo timu hiyo iliamua kumtumia kiungo Giresse kwenye nafasi hiyo ya kipa. Katika mchezo huo, Giresse alikuwa golini kwa dakika 60 na kuruhusu mabao matano kabla ya kutolewa na kuingizwa mchezaji mwingine wa ndani, Marius Tresor, ambaye alikwenda kutumika kwenye nafasi ya kipa. Hicho ndicho kitu cha kushangaza ilichofanya Bordeaux mwaka huo, 1982.

4) Jan Koller – Borussia Dortmund vs Bayern Munich, 2002

Wakati mwingine watu wanakuza tu mambo kwenye soka ikiwa kwamba inapaswa kuwa rahisi. Mfano, unapohitaji mchezaji wa ndani kuwa kipa, basi chaguo tu mwenye kimo cha kutosha kufanya hivyo na hilo ndilo walilofanya Borussia Dortmund mwaka 2002 kwenye mchezo wao dhidi ya Bayern Munich, ambapo walimtumia straika Jan Koller kuwa kipa wao. Straika huyo, mwili jumba ambaye utotoni alikuwa kipa, alichukua mikoba kukaa golini baada ya Jens Lehmann kuonyeshwa kadi nyekundu zikiwa zimebaki dakika 24. Mechi hiyo, Bayern ilishinda 2-1, lakini bao la Dortmund lilifungwa na Jan Koller kabla hajaenda kukaa golini.

3) Niall Quinn – Man City vs Derby, 1991

Niall Quinn anapenda sana kuwa kipa na jambo hilo lilifanya mara mbili kwenye maisha yake ya soka, huku moja wapo ni pale Manchester City ilipokipiga na Derby mwaka 1991, ambapo kipa Tony Coton alitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu. Quinn alichukua glovu na kwenda golini na Derby ambayo ilikuwa inahitaji ushindi ili isishuke daraja, ilifurahia na kuona imebahatika siku hiyo. Shughuli ya kwanza ya Quinn ilikuwa kukabiliana na penalti na hakika aliokoa mkwaju wa Dean Saunders. Man City ilishinda 2-1, ambapo Derby ilifanikiwa kumfunga bao moja tu Quinn.

2) Pele – Santos vs Gremio, 1963

Ilikuwa kama mwanafunzi tu wa shule, ambaye anakuwa mzuri katika kila kitu – usafi, umaarufu, michezo na kupendeza, basi hivyo alivyokuwa Pele, wakati alipoamua kuwa kipa katika mechi moja dhidi ya Gremio 1963. Akiwa ameshafunga hat-trick kwenye mechi hiyo, kipa wao Gilmar alitolewa kwa kadi nyekundu. Pele alijitolea kwenda kuwa kipa na hakika alionyesha kiwango bora sana akiwa golini na kufanya wachezaji wenzake kumsifu na kusema Pele ni kama vile alikuwa anapaa golini.

1) Cosmin Moti – Ludogorets vs Steaua Bucharest, 2014

Wachezaji wa ndani wanapochukua majukumu ya kuwa makipa, wanachotazama wao ni ile tu milingoti mitatu, mpira usipite, lakini Cosmin Moti, ambaye alikuwa beki wa kati wa Ludogorets alikwenda golini kuwa kipa, alifanya mambo matamu zaidi kwenye mechi ya kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Steaua Bucharest baada ya kipa halisi Vladislav Stoyanov kutolewa kwa kadi nyekunndu. Baada ya matokeo kuwa 1-1, mechi hiyo ilihitaji kupigiana penalti kupata mshindi, ndipo Moti alipoonyesha maajabu yake, akidaka penalti mbili. Paul Pirvulescu na Cornel Rapa, ndio waliokosa, Ludogorets wakishinda kwa mikwaju 6-5 na kusonga mbale.